Ibrahim Kamwe Ajivua Ukatibu Mkuu TPBO

Ibrahim Kamwe Ajivua Ukatibu Mkuu TPBO

KATIBU Mkuu wa ‘Tanzania Professional Boxing Organisation’ (TPBO), Ibrahim Kamwe amejitoa  katika uongozi wa chama hicho cha ngumi kama kiongozi. Akizungumzia hatua hiyo Kamwe alisema ameamua kupumzika kufanya shughuli za TPBO na kurudi kwenye ufundishaji wa vijana na kuendelea na kampuni yake ndogo inayojulikana kama Bigright Promotion ambayo inajihusisha zaidi na utayarishaji wa matamasha na uandaaji wa mapambano ya ngumi.

“Kwa kuwa naupenda mchezo wa ngumi na nimefanya shughuli hii kwa muda mrefu licha ya kuibuka utata utata wa hapa na pale na yote hii kwa ajili ya kuuendeleza mchezo wa ngumi nchini, lakini imekuwa ni ngumu kwangu kuendelea na wadhifa huu. Nawashukuru maofisa wenzangu ambao wamekuwa wakinipa ushirikiano wa karibu katika utekelezaji majukumu yangu, ila kwa sasa najitoa katika uongozi na nitajihusisha na ngumi kivingine ikiwemo kuwaendeleza vijana na kuandaa mapambano madogo madogo ya kukuza vipaji,” alisema Kamwe.

Kiongozi huyo mwanzilishi wa Bigright ambaye ukiondoa mambo ya kichama mara nyingi amekuwa akiwaongoza maofisa wa chama hicho katika shughuli mbalimbali na mapambano mengi kama jaji mkuu, muhifadhi rekodi za mabondia na mshauri katika shughuli za kiufundi amekuwa mdau mkubwa wa masuala ya mchezo wa ngumi kwa muda sasa.