Shinyanga, Tanzania
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida robo tatu ya wanafunzi katika shule ya sekondari Uhuru iliyopo katika Manispaa ya Shinyanga wamezuiwa kufanya mitihani ya muhula wa pili kwa madai ya wazazi wao kushindwa kulipia michango mbalimbali.
Baadhi ya wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo waliozungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa walisema pamoja na kuzuiwa kufanya mitihani hiyo walimu wao waliwapa adhabu ya kukaa chini wakiwa juani na baadae walipewa kazi ya kumwagilia bustani wakati wenzao wachache wakiendelea na mitihani.
Mmoja wa wanafunzi hao (jina tunalo) alisema walielezwa na walimu wao kwamba ye yote ambaye hatokuwa amelipa ada na michango mbalimbali shuleni hapo ikiwemo mchango wa mlinzi hatoruhusiwa kufanya mitihani hiyo mpaka pale wazazi wao watakapokuwa wamelipa michango wanayodaiwa.
Mwanafunzi huyo alifafanua kuwa hata pale walipojaribu kuwaomba walimu wawaruhusu kufanya mitihani kwa vile suala la michango si jukumu lao bali la wazazi waligoma huku wakibeza agizo la serikali lililotolewa hivi karibuni la ‘matokeo makubwa sasa’ (Big result now).
“Tuliwabembeleza sana walimu waturuhusu kufanya mitihani hasa wale wa kidato cha nne na cha pili kwamba matokeo ya mitihani hiyo kwa kawaida hujumuishwa na matokeo ya mwisho ya kumaliza kidato cha nne na wale wa cha pili, waligoma,”
“Binafsi niliwaeleza kuwa hivi sasa serikali imetangaza mpango wa matokeo makubwa sasa, lakini walimu hao walibeza na kueleza bila michango kulipwa hakuna Big results now, tulishangaa, tukaambiwa wote ambao hatujalipa michango na ada tukae chini uwanjani, hawakujali jua, kisha tukapewa kazi ya kumwagilizia bustani,” alieleza mwanafunzi huyo.
Kwa upande wake mkuu wa shule msaidizi Kasuka Masanja alikiri kuzuiwa kwa watoto hao kufanya mitihani kutokana na wazazi wao kutokulipa michango waliyotakiwa kulipa lakini hata hivyo alidai mitihani hiyo siyo halisi bali ilikuwa ni majaribio ili kuwashinikiza wazazi kulipa ada na michango wanayodaiwa.
Akizungumzia hali hiyo ofisa elimu sekondari manispaa ya Shinyanga Victor Emmanuel alishangazwa na taarifa za watoto hao kuzuiwa kufanya mitihani yao na kwamba ni kinyume na maelekezo yaliyotolewa na serikali.
“Siamini kama kweli wanafunzi hao wamezuiwa kufanya mitihani yao, si utaratibu, suala la michango haliwahusu watoto, ni la wazazi na tuliishatoa maelekezo ya jinsi ya kufuatilia michango hiyo kwa wazazi kwa utaratibu wa kuwasiliana na viongozi wa serikali katika kata, hairuhusiwi kabisa watoto kurudishwa nyumbani kwa kutolipa ada ama michango,” alieleza Emmanuel.
Hata hivyo Emmanuel aliahidi kulifuatilia tatizo hilo ili kuweza kubaini ukweli wake ambapo alitoa wito kwa shule nyingine kutozuia wanafunzi kufanya mitihani yao kwa sababu ya wazazi wao kushindwa kulipa ada ama michango au kuwapa adhabu ya aina yoyote kwa makosa ambayo siyo ya kwao.
Chanzo: theNkoromo Blog