WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema jitihada zaidi zinatakiwa kufanyika ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya nyuki hapa nchini na kufikia angalau asilimia 50 ya uwezo ilionao wa kuzalisha tani 140,000 za asali na tani 10,000 za nta kwa mwaka.
“Mapori yote nchini pamoja na maeneo ya kilimo yana uwezo mkubwa wa kuzalisha mazao ya nyuki kwa wingi. Ushiriki wa sekta binafsi katika uzalishaji na uwekezaji katika viwanda bado ni mdogo hivyo nahimiza na kuamini kuwa ushiriki wa sekta binafsi ni chachu kubwa katika kukuza sekta hii ya ufugaji nyuki,” alisema.
Alitoa kauli hiyo Agosti 30, 2013 wakati akizungumza wahitimu, wakufunzi na wazazi waliohudhuria mahafali ya kwanza na ya pili ya Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki cha Tabora yaliyofanyika kwenye viwanja vya chuo hicho.
Jumla ya wanafunzi 68 wamehitimu vyeti na stashahada ikiwa ni wahitimu wa mwaka 2011/2012 na 2012/2013 tangu kurejeshwa rasmi kwa mafunzo hayo kwenye chuo hicho cha Tabora kutoka Chuo cha misitu cha Olmotonyi kilichopo Arusha.
Waziri Mkuu alisema katika kipindi cha miaka minne iliyopita, kuanzia mwaka 2009 hadi 2012, uzalishaji wa asali hapa nchini ulifikia wastani wa tani 8,747 na wa nta ulifikia tani 583 kwa mwaka ambayo ni sawa na asilimia saba tu ya uwezo ambao nchi hii inao.
Alisema Tanzania ni moja kati ya nchi tano za Afrika zilizoruhusiwa kuuza asali yake katika soko la Umoja wa Nchi za Ulaya. Nchi nyingine ni Ethiopia, Zambia, Cameroon na Uganda. Alisema Ethiopia ndiyo inayoongoza kwa uzalishaji katika Afrika ikifuatiwa na Tanzania.
“Roho inaniuma ninaposikia kwamba Ethiopia ndiyo inaongoza kwa uzalishaji wa mazao ya nyuki barani Afrika. Wao wana jangwa kubwa tu, sisi tuna misitu kibao na maji ya kutosha. Lazima tujiulizie ni wapi tulikosea kwa sababu Tanzania ilikuwa inaongoza kwa uzalishaji kwenye miaka ya 60,” alisisitiza.
Ameutaka uongozi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki cha Tabora pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii wajipange na kuona namna ya kuinua uzalishaji huu. “Mkipata mitambo kidogo tu ya kusindika asali mtakuwa na nafsi kubwa ya kuwa wauzaji wakubwa wa asali nje ya nchi… wanunuzi wa nje wanataka traceability, ni rahisi kwa chuo kufanikiwa katika hili,” alisema.
“Soko lipo na bei nzuri. Tutumie fursa hii kuuza mazao yetu ndani na nje ya nchi ili kuongeza kipato cha kaya na cha Taifa kwa ujumla. Kama Asali inayozalishwa nchini itafungashwa vizuri kitaalam, kuna soko kubwa katika miji mikubwa, mahoteli, mashirika ya ndege, migodini na kwenye vituo vya utalii,” alisema.
Aliwataka wahitimu wa Chuo hicho watambue kwamba mafanikio katika maisha yao hayatategemea tu elimu ya ufugaji nyuki waliyojifunza, bali yatatokana na jinsi watakavyoitumia elimu hiyo kwa vitendo. “Elimu yenu ni zana, ni silaha, kwa hiyo itumieni vizuri. Ni silaha ya kuajiriwa, kujiajiri au kuwaajiri wengine katika miradi ya ufugaji wa nyuki, uzalishaji wa asali na nta na hatimaye kuleta maendeleo yenu binafsi na ya jamii nzima kwa ujumla,” aliwasihi.
Mapema, akitoa salamu za Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho, Kaimu Mwenyekiti, Bw. Liana Hassan aliiomba Serikali ikisaidie chuo hicho kupata sh. milioni 37/- ili kiweze kukamilisha mitaala yake kwa kuzingatia vigezo vya NACTE. Alisema kukamilika kwa hatua hiyo, kutakiwezesha chuo hicho kupata ithibati yake mapema.
Kuhusu changamoto zinazokikabili chuo, Bw. Hassan alisema miundombinu ya chuo haitoshi, madarasa hayatoshi, mabweni yamechakaa, na kwamba wanahitaji vifaa vya kisasa ili waweze kupata tarifa kupitia njia ya mtandao (internet).
Kuhusu tatizo la usafiri, Bw. Hassan alisema chuo kina gari moja tu ambalo ni la muda mrefu sana. “Tunaomba kupatiwa minibus mbili za wanafunzi, Land-Cruiser pick-up mbili ili zisaidie kubeba mahema na vifaa vingine wakati wanafunzi wakienda porini kimasomo na Land-Cruiser station wagon mbili kwa ajili ya idara ya utawala,” alisema.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Bibi Fatma Mwassa wakati akitoa salamu za mkoa huo kwa wahitimu aliwaasa wasisubiri kazi za kuajiriwa bali wafikirie kujiajiri kwani mafunzo waliyohitimu yanawapa fursa hiyo. Alitoa ofa ya mizinga ya nyuki kwa vijana 10 wa kutoka Tabora watakaojiunga pamoja na kuamua kuanzisha manzuki (apiary) yao ili kujiletea maendeleo.