*Yawaunga mkono wakulima wa shayiri na ngano mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara
Wakulima wa kanda ya kaskazini katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara wamenufaika kupitia kampuni ya bia ya Serengeti baada ya kampuni hiyo kuwapatia pembejeo bora na za kisasa pamoja na kuwahakikishia soko la uhakika kwa ajili ya bidhaa zao kwa kununua mazao yao kwa bei yenye kukidhi mahitaji ya wakulima hao. Hayo yalibainishwa baada ya kampuni hiyo kuwatembelea wakulima hao na kujadili changamoto, fursa na mikakati mbalimbali ya wakulima hao.
Wakulima hao wakiwa na furaha kubwa walibainisha kuwa kampuni ya bia ya Serengeti imekuwa ni mkombozi mkubwa sana kwao kwani kampuni hiyo imekuwa na ahadi za kweli kwa wakulima hao kwa kuwapatia mbegu za kisasa, kuwalipa kwa wakati na kikubwa zaidi kuwajali kwani suala la kuwatembelea na kujadiliana nao juu ya changamoto zinazowakabili na kutoa suluhisho la matatizo hayo ni ushahidi tosha kwamba kampuni ya bia ya Serengeti inawajali wakulima na kuonesha kuunga mkono juhudi za serikali katika kuendeleza kaulimbiu ya kilimo kwanza nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Kampuni ya Bia ya Serengeti, Meneja kilimo wa kampuni hiyo Shafii Mndeme alisema, “Hadi kufikia mwaka 2017 tunahitaji Tani 30,000 za shayiri na mpaka sasa tumepata tani 3000 tu za zao hili la shayiri, uhitaji bado ni mkubwa sana. Wito wangu kwa wakulima ni kujikita katika zao hili kwa kufuata maelekezo ya kilimo cha kisasa na kuotesha mbegu kwa wakati. Katika kuunga mkono juhudi za serikali yetu ya Tanzania katika sera ya kilimo kwanza, tunahitaji wakulima zaidi ya 100 na kwa sasa tumeanza na wakulima wa zao la shayiri katika mikoa ya kaskazini na mtama mweupe kwa mikoa ya kanda ya kati kwa kuwapa pembejeo za kilimo na soko la uhakika kwa mazao yao. Tunampango wa kuanzisha bidhaa inayotokana na zao la muhogo hivyo mkoa wa Mtwara na Mbeya wakae mkao wa kula”.
Kampuni ya bia ya Serengeti inajivunia kutumia malighafi za hapa nchini kuzalisha vinywaji vyake. Pia kampuni hiyo inatumia malighafi za Tanzania katika viwanda vyake nchini Kenya na Uganda hivyo kupanua wigo wa soko la shayiri Afrika Mashariki. Bwana Mndeme alitoa wito kwa serikali kuwa Serikali ipunguze ushuru kwa wakulima wanapopeleka mazao yao sokoni ili kuwafanya wakulima waweze kunufaika na kilimo kwa kupata mapato yatakayokidhi mahitaji yao. Pia serikali izifikirie kampuni mbalimbali nchini zinazowasaidia wakulima na kuwapunguzia kodi ili waweze kusaidia wakulima wengi zaidi nchini.
Naye diwani wa kata ya Ngare Nairobi wilayani Siha, Daniel Sandawa ambaye pia ni mkulima wa zao la shayiri Magharibi mwa mkoa wa Kilimanjaro alisema, “kwaniaba ya wakulima wa Ngare Nairobi tunaipongeza sana Kampuni ya bia ya Serengeti kwa ushirikiano na msaada mkubwa wanaotupatia katika kuendeleza kilimo cha shayiri. Kwani mkulima anapopeleka shayiri sokoni hulipwa ndani ya siku 14 kwa bei ya Tsh. 850 kwa kilo ambapo awali haikuwa hivo kwa kampuni zingine tulizowahi kufanya nazo kazi”.
Akiongea kutoka mashamba ya Basutu wilayani Hanang mkoani Manyara, Emannuel Hhawu Axwesso ambae pia ananufaika na mradi huu wa Kampuni ya Bia ya Serengeti, “tulikata tamaa kulima zao hili la shayiri kwani wakulima wadogo walikuwa wakinyanyasika katika swala la mgawanyo wa pembejeo na bei sokoni wakati wa kuuza mazao yetu. Tunaipongeza Kampuni ya Bia ya Serengeti kwa kujali wakulima wa aina zote bila kujali kuwa ni mkulima mdogo au mkubwa. Hii inatupa moyo wakuendelea kulima zao hili na tunaahidi kuongeza uzalishaji wa shayiri endapo changamoto tulizonazo zikitatuliwa.Tunahitaji vifaa vya kisasa zaidi, utafiti wa kina wa aina ya udongo katika mazingira yetu ili kujua ni aina gani ya mbolea inaweza kutuletea mazao mengi zaidi ”.
Changamoto hizo za wakulima zilijibiwa na Meneja kilimo wa Kampuni ya Bia ya Serengeti bwana Mndeme, ambapo alisema mwanzoni mwa mwezi Septemba wataalamu wa kilimo kutoka `International Crop Care’ kutoka nchini Kenya watakuja kufanya utafiti katia maeneo ya Kilimanjaro Magharibi na tayari wameshaingia mkataba na wakala wa mbolea ambayo itapendekezwa na wataalamu hao.