Kutoelewana Kati ya Rwanda, Tanzania Hakutavunja EAC

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk. Richard Sezibera

Na Balthazar Nduwayezu, EANA

KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC), Dk Richard Sezibera amesema hali ya sasa ya kutoelewana kwa muda mfupi kati ya Rwanda na Tanzania hakutavuja jumuiya hiyo yenye wananchama watano.
Licha ya Rwanda na Tanzania wananchama wengine wa jumuiyo hiyo ni pamoja na Kenya, Uganda na Burundi.

“Kutoelewana si jambo zuri kwa Jumuiya, lakini sidhani kama kuna hatari ya kuvunjika kwa jumuiya kuhusu jambo hili, hapana!,” Dk. Sezibera alisisitiza katika mkutano na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya jumuiyo hiyo jijini Arusha Jumatatu.

“Jumuiya hii ya sasa ni tofauti na ile ya awali. Mkataba uko wazi kabisha juu ya uendeshaji wa masuala mbalimbali, kazi ya Jumuiya inaendelea na serikali hizi mbili zipo katika majadiliano juu ya mambo mbalimbali,” alisema Dk Sezibera.

Dk. Sezibera alikuwa anajibu maswali ya waandishi wa habari juu ya hali ya ‘mvutano’ kati ya nchi mbili hizo wananchama wa EAC, Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) linaripoti.

Sintofahamu ilianza wakati Tanzania ilipotoa wanajeshi wake kwa brigedi ya Umoja wa Mataifa (UN) kwa ajili ya Juhudi za Kuleta Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (MONUSCO) yenye jukumu la kupambana na kuwanyang’anya makundi ya waasi yenye silaha Mashariki mwa nchi hiyo. Moja kati ya makundi hayo ni M23 ambalo linadaiwa kuungwa mkono na Rwanda.

Mvutano uliongezeka wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika (AU) ambapo Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania alizishauri Rwanda na Uganda kufanya mazungumzo na wahasimu wao kama Jamhuri wa Kidomkroasia ya Congo (DRC) inavyofanya, ili kuleta suluhishio la kudumu la amani na umoja katika Ukanda wa Maziwa Makuu.

Rwanda ilikasirishwa na pendekezo la kufanya majadiliano na kundi la kijeshi la FDLR, ambalo linadaiwa kuwa na makao yake Mashariki mwa DRC na ambalo Rwanda linalituhumu kuchochea mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

Tangu wakati huo kumekuwepo kurushiana maneno baina ya serikali zote mbili na vyombo vya habari na  wakati mwingine maneo makali yalikuwa yakitumika, kiasi cha kuleta hofu ya uwezekano wa kuzuka vita kati ya nchi hizo mbili rafiki.