Membe Awatetea Watanzania Waishio Nje Maoni Katiba Mpya

Waziri Mkuu Mstaafu wa Zamani, Dk. Salim Ahmed Salim akifungua Baraza la Katiba la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika mchakato wa mabadiliko ya Katiba lililofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dares Salaam. Picha Eleuteri Mangi –maelezo.

Na Magreth Kinabo na Eleuteri Mangi, Maelezo Dar es Salaam

BARAZA la Katiba la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa limependekeza kuwa Watanzania waliopo nje ya nchi wasifutiwe uraia wa Tanzania.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Mambo Nje ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe wakati alipokuwa akichangia suala la uraia katika mchakato wa mabadiliko ya Katiba kupitia baraza hilo kwenye ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

“Raia wa Tanzania aliyeko nje ya nchi na kuomba uraia wa nchi hiyo kwa sababu yoyote ile iwe ya elimu, afya au ajira asifutiwe uraia wa Tanzania,” alisema Waziri Membe.

Waziri Membe aliongeza kuwa Watanzania waliopo nje ya nchi ambao ni waaminifu hawawezi kupata ajira rasmi ‘white collar job’ hivyo kishia kufanya kazi zisizo rasmi. Alifanunua kwa Watanzania walioamua ‘kujilipua’ yaani kuukana uraia wamepata kazi nzuri lakini hawasaidii taifa lao la asili.

Kauli hiyo ya Waziri Membe iliungwa mkono wa baadhi ya mabalozi waliotumikia Tanzania katika nchi mbalimbali wakati mjadala huku wakitaka suala liwekewe utaratibu ili kuokoa nguvu kazi ya taifa na wataalamu mbalimbali walioko nje ya nchi.

Miongoni mwa mabalozi waliounga mkono ni Balozi Martin Lumbanga ambaye alisema “Suala la uraia wa nchi mbili ninaliunga mkono kwa kuwa lina faida nyingi kuliko hasara,” alisema.

Balozi Paul Rupia alisema ni wakati umefika kwa Watanzania kuwa na uraia wa nchi mbili, hivyo suala hilo lisiogopwe bali liwekewe utaratibu unaofaa.

“Ni vema tuliwekee utaratibu ili tuendelee kuwa na watu wetu bila kuwapoteza,” alisema Balozi Rupia.

Kwa mujibu wa Waziri Membe alisema hivi sasa Watanzania waliopo nje ya nchi ni milioni tatu kati ya Watanzania zaidi milioni 44. Baraza hilo lilihudhuriwa na mabalozi hao, makatibu wakuu kiongozi wastaafu, na watumishi mbalimbali wa wizara hiyo ambapo aliazimia suala hilo liingizwe kwenye mchakato wa rasimu ya Katiba.