Ushauri wa Bure Kwa Msanii Dully Sykes na Watanzania Wenzangu!

20130826-124153.jpg

Mwanamuziki mkongwe wa Bongo Fleva, Dully Sykes

Jana nilitembelea mtandao wa Ankal Michuzi (ndio wana Blogu huwa tunatembeleana kubadilishana uzoefu -:))na baada ya kupita hapa na pale, nikakumbana na habari, iliyoambatana na video tatu kutoka Tanzania Film Critics Association (TFCA). Video hizi http://issamichuzi.blogspot.de/search?updated-max=2013-08-25T12:49:00%2B03:00 zilikuwa za mahojiano ya wasanii watutu, yaani John Kitime, Dr. vicensia Shule, na Dully Skyes. Sikuwa na muda mwingi kutokana na majukumu ya kazi, hivyo niliweza kuangalia video mbili tu mpaka mwisho, nazo ni ile ya John Kitime na Dully Sykes. Baada ya kuangalia video za mahojiano hayo yaliyohusu sheria ya ushuru wa bidhaa, sura 147, nilishindwa kujizuia na hivyo kulazimika kuandika maoni yafuatayo (chini) kwenye blog ya michuzi kwa maslahi ya Msanii wetu mahiri Dully Sykes na Watanzania wenzangu:

Maoni haya nimeyaongeza kidogo, ili kukidhi mahitaji ya mtandao wetu na wasomaji wake.
…………………………………………..

Dully Sykes, kwanza napenda kuanza kwa kusema kwamba nakuheshimu kama miongoni mwa wanamuziki wa mwanzo wa Bongo Flava, ambao mmechangia sana kuukuza mziki wetu huu tuupendao, na hongera sana kwa kuendeleza mapambano mpaka sasa, kwani miaka 17 ya muziki si haba!

Baada ya hayo, ni muhimu nikaweka wazi kwamba maelezo yako katika mahojiano haya, yamenisikitisha sana, yaani unaonekana ni mtu wa lawama na kutaka kusaidiwa tu, bila kuwa tayari kubeba majukumu yako binafsi katika kuhakikisha maslahi yako yanalindwa.

Nazungumzia ‘responsibility’, ambayo hauonyeshi kuwa nayo, kwa mfano, haujui hata alama zinazotumika kulinda kazi zenu, na wala haujui kazi za wasanii zinalindwa vipi (wakati wewe ni msanii)???? Ukiulizwa kwanini, unasema “Mimi sijapata elimu yeyote na wala sikuitwa” sasa kwanini usifuatilie mwenyewe na kuweza kujielimisha na kujilinda? Maana mwisho wa siku, ni wewe ndio unayeibiwa na si BASATA wala COSOTA. Au ina maana ukongwe wako katika muziki huu na jina lako kubwa vina kuzuia kuwa fuata watu, mpaka ufuatwe au uitwe?

Amka Dully na wasanii wengine kwa kujielimisha wenyewe kwa kufuata hizo elimu zilipo na si kusubiri tu “kuelimishwa” na kusaidiwa na serikali na maadvocate!

Natambua kwamba mnafanya kazi katika mazingira magumu sana, maana wasanii wanashindwa kunufaika na kazi zao ipasavyo kutokana na wizi uliokithiri. Lakini, ufumbuzi wa tatizo hili hauwezi kupatikana bila wasanii wenyewe kuchukua jukumu la kujielimisha na kufuatilia mambo yote yanayohusiana na ulindaji wa kazi zao, kwani mhusika wa kwanza ni msanii mwenyewe. Kama msanii upo busy kiasi cha kushindwa kufuatilia masuala haya, basi bila shaka upo busy unatengeneza pesa.

Kwahiyo basi, hakikisha kwamba una Meneja makini, ambaye atafuatilia masuala haya kwa niaba yako na baadae fursa ikipatikana mnakutana ili akuelimishe na wewe pia. Ni jitihada hizi tu ndio zitakazo tunasua katika janga hili.

Huu ni ushauri kwa Watanzania wenzangu wengine wengi tu katika nyanja mbalimbali, ambao tumezoea kulalamika, bila kuchukua hatua zipasazo kumaliza matatizo yetu. Kwa mfano, Ndg. John kitime katika mahojiano yaleyale, ambayo alifanyiwa Dully Sykes pia. Yeye alisisitiza suala la umoja, yaani kuanzisha vitu kama vyama vya wafanyakazi, wasanii, na kadhalika….katika kudai maslahi yetu. Hili ni muhimu sana na ninaliunga mkono kwa nguvu zote, kwani kinachoendelea sasa miongoni wa wasanii na wengineo ni mparaganyiko, ambao unaacha pengo kubwa katika uwakilishi wa matatizo. Kama watu watajielimisha na kuwa pamoja, serikali italazimika tu kusikiliza na kuchukua hatua dhidi ya matatizo husika.

Lakini serikali ikiona mgawanyiko na uelewa mdogo, basi ina kuwa rahisi kwake kulifumbia macho suala fulani au kugeuza mradi wa maslahi ya wachache.

Ni ushauri wa bure tu.

Asanteni,

Rungwe Jr.