Nahitaji Kuonana na Rais Kikwete…!

Edson Kamukara


Na Edson Kamukara

UJUMBE wangu uko wazi na uanaeleweka kwa kila mtu kwamba naomba kuonana ana kwa ana na Rais wetu Jakaya Kikwete potelea mbali hata kama wasaidizi wake wataona sina hadhi ya kukanyaga Ikulu, watanikutanisha naye popote.

Sitanii katika hili kwani nimebaini makala zangu zote nilizoandika kushauri na kuhoji masula mbalimbali, wasaidizi wake hawazifikishi taarifa hizo kwake badala yake wananipigia simu za vitisho kuwa namwandika vibaya mkuu wa nchi.

Hivyo naleta maombi yangu rasmi leo kwa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, nikiomba kuandaliwa nafasi ya kuonana na rais wetu ili nimfikishie ushauri wangu juu ya maswala kadhaa yanayolihusu taifa letu.

Najua uwezekano huo wa kukutana naye upo kama wasaidizi wake hawatafanya mtima nyongo. Maana nimemwona mara kadhaa akikutana na watu mbalimbali Ikulu kama wanamichezo, wasanii, vijana walioacha kutumia dawa za kulevya, wanasiasa na wengineo. Kumbe nami nastahili.

Niweke wazi kuwa siendi kujipigia debe ya kuomba madaraka, kipaji hicho cha unafiki wa kujipendekeza kwa wakubwa ili wanikumbuke kimasilahi sijabahatika kukipata, zaidi natazama mustakabali wa Tanzania na watu wake.

Ajenda zangu za kujadiliana na rais ni zile zile nilizoandika miaka yote pasipo wasaidizi wake kumfikishia. Moyo unauma kuona nchi yangu inaangamia wakati kiongozi tuliyemkabidhi nchi alituahidi kupambana kwa Ari, Nguvu na Kasi mpya (ANGUKA).
Kwa wale ambao hawana desturi ya kuweka kumbukumbu za kauli za viongozi wetu, Desemba 30 mwaka 2005, Rais Kikwete wakati akilihutubia Bunge kwa mara ya kwanza alitoa hotuba ndefu ya zaidi ya saa mbili na kuahidi mambo lukuki.

Kwa uchache kupitia kwa wawakilishi wetu bungeni (wabunge) aliahidi kupambana na rushwa, dawa za kulevya, uhalifu nchini, ajira kwa vijana kwa kauli mbiu ya ‘ANGUKA’.
Tena katika kuwaonesha wabunge kuwa yuko ‘serious’ alisema anaweza akawa anacheka lakini mkali katika kutenda. Kauli hii ilinivutia kutokana na ukweli kwamba wananchi wengi kumwona Rais wetu kama kiongozi wenye furaha, rafiki wa kila mtu na hivyo kudhani hawezi kuwashughulikia wavunja sheria.

Kwa hiyo ajanda yangu kwa rais itakuwa kumkumbusha hotuba ile na kutaka kujua ameitekeleza kwa kiwango gani ikizingatiwa kuwa rushwa aliyotuahidi kuitokomeza sasa imekithiri kila sehemu hata kwenye vyombo vya sheria vinavyotoa haki kwa watu.

Dawa za kulevya, umekuwa wimbo ambao kila mtu leo hataki kuusikia kutokana na kujirudia kila sekunde. Zimeharibu maisha ya nguvu kazi ya vijana nchini na sasa wauzaji wameamua kuvuka mipaka na kutuchafulia jina ya Taifa nje ya nchi wanakokamatwa baada ya kupita kilaini kwenye mipaka yetu.

Nitamkumbusha zile ajira za vijana “Machinga” alioahidi kuwajengea majengo ya kufanyia biashara zao kila wilaya (Machinga Complex) kuwa ni kupoteza muda na rasilimali bure kwani hiyo si njia ya kuwasaidia vijana kujikwamua.

Nitafichua ukweli kuwa machinga wetu wanafanya kazi ya kuwasaidia wafanyabiashara wakubwa kukwepa kodi kwa kuuza bidhaa mitaani, hii ndio sababu wao kila wanapotengewa maeneo maalum na kujengewa vizimba hawakanyagi kwa vile wanajua watalipa kodi.

Si kwamba nitafanya hivyo nikiwa na lengo la kuwachongea mawaziri wake wenye dhamana ya vijana na ajira kuwa wameshindwa kazi la hasha. Mimi nitakuwa natoa ushauri ambao akiamua anaweza kuukataa.

Kwa mawazo yangu madogo na pengine ya kijinga, nitamdokeza kuwa njia pekee ya kutengeneza ajira kwa vijana wa tabaka hili la kati kielimu ni kuwa na vyuo vya Veta kila wilaya, kuanzisha viwanja vidogo kwenye maeneo mbalimbali ili badala ya kuuza mali ghafi, tuwe na viwanda vya uchakataji vitakavyoendeshwa na vijana.

Hatua hii kwanza itatuwezesha kuongeza thamani ya mazao yetu huku tukiwa tumetengeneza ajira nyingi huko huko vijijini badala ya kuwapumbaza vijana wetu kuwatela mjini na kuwageuza wachuuzi ili wawe mtaji wa kufanikisha ushindi wa watawala wenye fikra finyu zinazojali familia na koo zao.

Kama nitapata muda wa kutosha kuzungumza na rais, nitamkumbusha pia mchezo wa kisiasa unaofanywa katika utoaji wa elimu nchini kuanzia awali hadi chuo kikuu.
Niliwahi kusema huko nyuma katika makala zangu kuwa ukinunua nguo mpya inakusaidia kuongeza idadi ya nguo ulizonazo lakini haimaanishi kwamba zile za zamani unazichana au kuzitupa hata kama zina ubora kuliko hizo mpya ‘feki’.

Hapa nitamwambia kwamba shule kongwe zilizojengwa na wakoloni pamoja na zile za serikali kabla ya ufisadi kushika kasi, zilikuwa imara na bora na zimedumu hadi leo ambapo zile za kata zilizojengwa ndani ya muda usiofika miaka kumi zina nyufa za kutisha.
Hoja hapa ni kwamba fedha nyingi tulizozipoteza kujenga shule mpya za hovyo ambazo hazina walimu, vitabu, maabara, miundombinu bora, maktaba ni heri mara mia moja zingetumika kukarabati shule zile kongwe na kuziongezea majengo na mahitaji mengine zikapaokea idadi kubwa ya wanafunzi.

Nasisitiza kwamba nisieleweke vibaya kuwa wasaidizi wa rais katika nyanja hizo hawafai. Najua wanafanya kazi na uwezo wao umefikia hapo ila tunapaswa kusogea mbele kifkra tuitazame elimu ya juu ambayo serikali inagawa mikopo wanafunzi wasome ila wakimaliza hawana kazi.

Hawa watarudishaje mikopo kama serikali haiandai mazingira ya wao kuzalisha? Nisimalize yote hapa ila wasaidizi wa rais Kikwete tafadhali naomba nafasi niwasilishe haya kwake, nasubiri kujibiwa. Tafakari!