PINDA AWAALIKA WAWEKEZAJI WA GESI ASILIA KUTOKA NJE

Waziri Mkuu Mizengo Pinda

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amesema umefika wakati kwa wawekezaji wa kimataifa kuangalia uwezekano wa kuwekeza katika miundombinu ya kusafirisha gesi asilia kama njia mojawapo ya kusaidia kukuza uchumi wa Tanzania.

Amesema kupatikana kwa gesi nyingi katika ukanda wa pwani ya kusini mwa Tanzania kunatoa fursa ya wawekezaji kuanza kufikiria ujenzi wa mabomba ya gesi ili bidhaa hiyo iweze kutumika viwandani, kuendesha mitambo pamoja na viwanda.

Ametoa kauli hiyo Julai 8, 2011 kwenye hoteli ya Samsung mjini Geoje, wakati akiwahutubia wageni maalumu kutoka kampuni mbalimbali za wawekezaji waliohudhuria uzinduzi wa meli ya uchimbaji mafuta iitwayo Poisedon katika bandari ya Geoje, iliyoko Kusini Mashariki mwa Seoul, Mji Mkuu wa Korea Kusini.

“Tangu mwaka 1974 ilipogunduliwa gesi asilia katika kisiwa cha Songosongo katika pwani ya kusini mwa Tanzania, kumekuwa na ugunduzi mbalimbali kutokana na tafiti zilizofanywa na makampuni ya nje kwa kushirikiana na TPDC.”

“Miaka kadhaa baadaye, iligungulika akiba kubwa ya gesi asilia huko Mkuranga karibu na Dar es Salaam; ikafuatia Mnazi Bay mwaka 2007; Kiliwani mwaka 2008; na sasa kampuni ya Ophir kwa kushirikiana na kampuni ya British Gas wamegundua visima vitatu maeneo ya Mtwara… hii ni dalili njema kuwa Tanzania ina hazina (reservoir) kubwa ya gesi na mafuta,” alisema.

“Chini ya sera yetu ya mwaka 2010 ya Ushirikiano baina ya Umma na Sekta Binafsi, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na sekta binafsi, makampuni ya uchimbaji mafuta na gesi itabidi tutafute njia za kuleta ufanisi ili ugunduzi huu uweze kuimarisha sekta ya mafuta na gesi kuendeleza uchumi wa nchi yetu,” alisema.

“Kutokana na mipango ya baadaye tuliyonayo, sekta binafsi haina budi kujitokeza na kuangalia ni maeneo gani wanaweza kuwekeza katika uchimbaji mafuta na gesi na kwa kuanzia wanaweza kungalia usafirishaji wa gei na usambazaji wake, viwanda vya mbolea, kuleta magari yanayotumia gesi au kutengeneza injini za gesi zinazoweza kuzalisha umeme,” alisema.

Alisema hayo ni maeneo machache ambayo wanaweza kufikiria kuanza nayo katika uwekezaji wao wenyewe kama sekta binafsi au kwa kushirikiana na Serikali.

Kwa upande wa Petrobras, kampuni ya Brazil ambayo itaendesha utafiti nchini Tanzania, Waziri Mkuu alisema ana matumaini na kampuni hiyo kama mbia makini kutokana na historia ambayo imejiwekea duniani tangu mwaka 1952 ilipoanzishwa.

“Nimeambiwa kwamba mwaka jana, kampuni ya Petrobras ilikuwa na uwezo wa kuzalisha mapipa zaidi ya milioni mbili ya mafuta kwa siku… vilevile ni kampuni inayojulikana kwa kutumia teknolojia za kisasa kuzalisha mafuta kwenye maji ya kina kirefu,” aliongeza.

Mapema leo asubuhi, mke wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda na Bibi Anne Tollefsen walipewa kazi ya kubatiza meli mbili (kuwa mama wa ubatizo) zilizozinduliwa leo na kukata kamba kwa shoka kuashiria kutoa nanga kwa meli hizo. Meli hizo ni Poseidon inayokuja Tanzania na Mykonos inayoenda Brazili.

Mama wa ubatizo huteuliwa na kampuni inayomiliki meli, kwa hiyo walimteua Mama Tunu Pinda awe mama wa ubatizo wa meli ya Poseidon, na Bibi Anne Tollefsen awe mama wa ubatizo wa meli ya Mykonos. Bibi Tollefsen ni mke wa Afisa Mwendeshaji Mkuu wa kampuni ya Ocean Rig, Bw. Frank Tollefsen kampuni ambayo inasimamia ujenzi wa meli hiyo.

Leo mchana, (Ijumaa, Julai 8, 2011) Waziri Mkuu atatembelea eneo la Georim lenye viwanda vya kusindika mazao ya kilimo katika mji huu wa Geoje.

Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu amefuatana na mkewe Mama Tunu Pinda, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Balozi wa Tanzania nchini Japan, Bibi Salome Sijaona, Balozi wa Brazili nchini Tanzania, Bw. Francisco Carlos Luz, Mwenyekiti wa TPDC, Jenerali Mstaafu, Robert Mboma na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Bw. Yona Kilagane.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
IJUMAA, JULAI 08, 2011.