RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kuomboleza kifo cha mwanasoka za zamani nchini, Hayati Baraka Kitenge.
Katika salamu zake hizo, Rais Kikwete amesema kuwa amesikitishwa na taarifa za kifo cha Mzee Kitenge, mmoja wa wanasoka wa Tanzania ambao walichangia kwa kiasi kikubwa kukuza mchezo huo nchini.
“Nimesikitishwa na taarifa ya kifo cha Mzee Kitenge ambaye nimejulishwa kuwa alifariki dunia Jumatatu wiki hii na kuzikwa Agosti 21, 2013 katika makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam. Daima, tutamkumbuka Mzee Kitenge kama mwanasoka hodari na mmoja wanasoka waliochangia maendeleo ya mchezo huo nchini.”
“Kufuatia msiba huo, nakutumia wewe Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, salamu zangu za rambirambi kuomboleza msiba huo. Aidha, kupitia kwako, naitumia familia ya Mzee Kitenge pole nyingi nikijua fika majonzi na machungu yao katika kipindi hiki kwa kuondokewa na mhimili wa familia,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Kupitia kwao vile vile nawatumia rambirambi wanamichezo wote nchini hususan wanasoka, pamoja na viongozi na wanachama wa Klabu ya Dar Es Salaam Young Africans ambayo marehemu aliichezea kwa kipindi kirefu cha maisha yake. Naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke peponi roho ya Marehemu Baraka Kitenge. Amina.”