Rwanda Yaichokonoa Familia ya Rais Kikwete

Rais wa Rwanda, Paul Kagame

UHUSIANO kati ya Tanzania na Rwanda unazidi kudorora kutokana vyombo vya habari na baadhi ya maofisa wa nchi hiyo kuanza ‘kuichokonoa familia ya Rais Jakaya Kikwete’.

Tovuti ya News of Rwanda, imedai kuwa mke wa Rais, Salma Kikwete ni ndugu wa kiongozi wa zamani wa taifa hilo, Juvenal Habyarimana ambaye aliuawa kwenye ajali ya ndege wakati akitokea nchini Tanzania mwaka 1993.

Madai hayo yametokana na mtandao wa Wiki Leaks, ambao ulinasa mawasiliano kati ya Ubalozi wa Marekani nchini na Serikali ya nchi hiyo. Kadhalika taarifa hiyo ya Wiki Leaks imenukuliwa na magazeti mengine ya Rwanda likiwamo gazeti maarufu la New Times.

Hata hivyo, Msemaji wa Serikali ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene amekanusha taarifa hizo zinazodai kuwa Rais Kikwete ni shemeji yake na Habyarimana.

“Taarifa hizi hazina ukweli wowote na zinalenga kumpaka matope Rais Jakaya Kikwete,” alisema Mwambene.

Mwambene amefafanua kuwa lengo la mitandao ya kijamii ni kuhabarisha na kuelimisha umma na si kupotosha jamii kwa kuandika habari zisizo na ukweli wowote.

Kutokana na tovuti hiyo kuchapisha habari hiyo, wasomaji wake walitoa maoni mengi ya kumkashifu Rais Kikwete.

Baadhi yao walikwenda mbali zaidi kwa kuhusisha habari hiyo na uamuzi wa hivi karibuni wa kuwatimua raia wa Rwanda wanaoishi bila kibali nchini.

“Kama Mama Salma Kikwete ni binamu wa Habyarimana basi Rais Kikwete amrudishe nyumbani kwao Rwanda,” aliandika msomaji wa gazeti hilo, Osma Kanyambo. Hali hiyo ni mwendelezo wa vita vya maneno kati ya Tanzania na Rwanda, ambavyo vilianza tangu mwezi uliopita.

Chanzo cha hali hiyo ni ushauri uliotolewa na Rais Kikwete wa kuitaka Rwanda kuzungumza na kundi la waasi la FLDR ambalo limekuwa likiendesha vita kwa miaka 16 sasa wakiwa mafichoni katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Rais Kikwete katika hotuba ya mwisho wa mwezi uliopita alikiri kudorora kwa uhusiano kati ya Tanzania na Rwanda na kwamba nchi hiyo inamshutumu kutokana na ushauri aliowapa.

Rais wa Rwanda, Paul Kagame na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Louis Mushikiwabo walikaririwa kwa nyakati tofauti wa wakitoa kauli zenye mwelekeo wa kashfa kwa Rais Kikwete.

Hali imekuwa mbaya zaidi baada ya Rais Kikwete kuagiza operesheni ya kuwaondoa raia wa nchi jirani (Rwanda ikiwamo) wanaoishi nchini bila ya vibali.

Serikali ya Rwanda pekee ndiyo imepinga operesheni hiyo, ambayo imesababisha kuondolewa kwa raia wake wapatao 6,000 ambao walikuwa wakiishi nchini kinyume cha sheria. Nchi nyingine; Burundi, Uganda na DRC ambazo pia raia wake wameondolewa lakini hazikulalamikia operesheni hiyo.

Taarifa ya Weak Leaks
Taarifa hiyo ni ile iliyotumwa na ofisa mwandamizi wa Ubalozi wa Marekani nchini, Shabyna Stillman Mei 5, 2005 akidai kuwa Mama Salma ni binamu wa Habyarimana


CHANZO: www.mwananchi.co.tz