Operesheni Ondoa Wahamiaji Haramu Kuanza Kanda ya Ziwa

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu wahamiaji haramu waliorejea kwao baada ya agizo la Rais Jakaya Kiwete alilolitoa Juni 29, mwaka huu katika ziara yake ya Mkoa wa Kagera.


Kamishina Mkuu wa Uhamiaji, Magnus Ulungi wa kwanza kulia mstari wa mbele na Ofisa Uhamiaji Mrakibu Bi. Rosemary Mkandala wakiwa katika mkutano wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu wahamiaji haramu waliorejea kwao baada ya agizo la Rais Jakaya Kiwete alilolitoa Juni 29, mwaka huu katika ziara yake ya mkoa wa Kagera (Picha na Lorietha Laurence –Maelezo)

Na Magreth Kinabo – MAELEZO

SERIKALI imesema operesheni ya kuwaondoa wahamiaji haramu katika Kanda ya Ziwa itaanza kwa kushtukiza, huku ikiendelea kusisitiza watu wanoaishi nchini bila taratibu za kisheria kuondoka kwa hiari na mali zao.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wahamiaji haramu waliorejea kwao baada ya agizo la Rais Jakaya Kiwete alilolitoa Juni 29, mwaka huu katika ziara yake mkoani Kagera.

“Nimeshapewa maelekezo rasmi na Rais Jakaya Kikwete ya kuwaondoa wahamiaji haramu nitakapoona inafaa. Operesheni itaanza kwa kushtukiza. Muda muafaka wa kutekeleza vyombo vya dola vitasema.

“Tunatoa wito waondoke wenyewe na mali zao bila kunyang’nywa. Wenye mali nyingi wanatakiwa kutoa taarifa katika vituo vya polisi ili waweze kusindikizwa. Hatutawavumilia wahamiaji haramu,” alisema Waziri Nchimbi.

Aliongeza kuwa wahamiaji hao wanaotaka kuishi nchini kihalali wanatakiwa kurudi nchini kwao kwanza na kufuata taratibu za kisheria kama ambavyo nchi nyingine zinavyofanya mtu akitaka kuishi nchi yoyote anatakiwa kufuata taratibu hizo.

Waziri alitoa onyo kwa viongozi wa vijiji wanaoshirikiana na wahamiaji hao kuwatunza na kusema jambo hilo ni makosa kisheria, hivyo watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumzia kuhusu takwimu za wahamiaji hao waliorejea nchini kwao mpaka sasa ni 10,672 kati ya hao Wanyarwanda ni 6,088, Warundi 4000 na Waganda 269 ambao wametoka Mkoa wa Kagera. Kwa Mkoa wa Kigoma ni Warundi 142, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo nane na katika mkoa wa Geita Wanyarwanda 126 na Warundi 39.

Hata hivyo Waziri Nchimbi alisema kuna wahamiaji 14 wamerejea nchini tena baada ya kurudi makwao na kuwataka wasilione jambo hilo kuwa ni mzaha.

Aidha Waziri Nchimbi alisema Serikali ya Tanzania inashukuru kwa ushirikiano unaotolewa na nchi wanazotoka wahamiaji hao kwa kuwapokea vizuri.

Alifafanua kuwa suala la kuwarudisha wahamiaji hao si la mara ya kwanza, lilishawahi kutokea. Huku akisisitiza kwamba tatizo linatokana na sababu mipaka yetu mikubwa na kuna watu wasio wazalendo ambao wanawapokea na kuwakaribisha kwa kupatiwa zawadi. Hivyo Serikali inalifanyia kazi jambo hilo.