MKE wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda amesema kuna haja ya kuweka juhudi za makusudi za kuwawezesha wasichana wote nchini kuondokana na aibu zinazowazuia kuhudhuria masomo yao kila siku.
Amesema kukosekana kwa vifaa vya kujisetiri miongoni mwa wasichana waliofikia balehe, ni miongoni mwa sababu zinazowafanya wakose masomo kati ya siku 30 hadi 70 kwa mwaka jambo ambalo linachangia kudorora kwa elimu miongoni mwao.
Ametoa kauli hiyo Agosti 20, 2013 wakati akizindua Mradi wa Hakuna Wasichoweza katika Shule ya Msingi Chilongola, iliyoko Manispaa ya Mtwara Mikindani, mkoani Mtwara. Mradi huo unafadhiliwa na Taasisi ya T-MARC inayojihusisha na Masuala ya Afya na Maendeleo, umelenga kuwafikia wasichana 10,000 katika wilaya mbili za mkoa wa Mtwara, yaani Manispaa ya Mtwara Mikindani na Wilaya ya Mtwara Vijijini.
“Wasichana wengi wanapopata siku zao, hushindwa kuhudhuria masomo yao kati ya siku tatu hadi saba kwa mwezi au siku kati ya siku 30 hadi 70 kwa mwaka. Hii husababishwa na wasichana hawa kukosa nyenzo za uhakika za kujisitiri wakiwa shuleni. Wengi wao huamua kubaki nyumbani hadi pale mizinguko yao itakapokwisha ili kuepuka kuaibika…,” alisema.
Alisema usiri na ufahamu mdogo wa jamii kuhusu masuala ya hedhi na changamoto wanazozipata wasichana katika kipindi hiki pia ni tatizo kubwa. “Wengi wetu katika jamii inayotuzunguka bado tunalichukulia suala la hedhi kuwa suala la aibu na la siri kubwa, kwa hiyo matatizo yanayotokana na hali hii ya kawaida hubaki bila kushugulikiwa, kwani kila mtu anaona aibu kusema wazi kuwa kuna tatizo,” aliongeza.
“Kwa vile hedhi hazichagui siku maalum, inawezakana kabisa kuwa siku hizo za shule wanazokosa wasichana hawa zikawa ni siku za mitihani ama za masomo muhimu. Matokeo yake ni wasichana kukosa vipindi, na walimu huwa hawarudii vipindi kwa ajili ya wale waliokosa vipindi,” alisisitiza.
Alizitaja sababu nyingine zinazochangia tatizo hilo ni kukosekana kwa maji safi na huduma safi za vyoo ikiwemo milango ili kulinda heshima ya mtumiaji. “Huduma za vyoo na maji safi ni changamoto nyingine kubwa inayozikabili shule zetu. Shule nyingi hazina vyoo vya kutosheleza idadi ya wanafunzi waliopo na hata hivyo vichache vilivyopo, mara nyingi havina milango ya kulinda heshima na usiri wa mtumiaji, au hata maji na sabuni ya kujisafisha,” alisema.
Alisema changamoto nyingine iliyopo ni kukosekana kwa elimu ya kutosha miongoni mwa wasichana wengi walio kwenye umri wa kubalehe, kunawafanya washindwe kujitambua na kutambua mabadiliko yanayotokea katika miili yao.
“Ukosefu huu wa ufahamu pamoja na mahitaji mengine ya maisha, umewafanya wasichana wengi kuwa chambo kwa wanaume ‘mafataki’ wanaowalaghai kwa urahisi. Idadi kubwa ya mimba katika umri mdogo na kasi kubwa ya maambukizi ya magonjwa ya ngono na Virusi vya UKIMWI (VVU) miongoni mwa wasichana wa umri huu ni uthibitisho tosha wa tatizo hili,” alisema.
Aliipongeza TMARC kwa kuzindua mradi huo ambao umelenga kuinua mahudhurio shuleni na ufaulu miongoni mwa wanafunzi wa kike.