YAFUATAYO ni maazimio ya Mafunzo ya kamati za Bunge zinazosimamia fedha za umma na bajeti (PAC, LAAC NA BC)
1.) Kutokana na kutokuwepo na taarifa sahihi kuhusu deni la Taifa kuna umuhimu wa
kukutanisha wadau wakuu wanaohusika hususani BOT, HAZINA, Kamati za Bunge na CAG
ili kuweza kujua kwa usahihi zaidi ukubwa wa deni hilo. Vile vile imeamuliwa
kuwa Serikali ishauriwe kuunda chombo huru kitakachosimamia deni la taifa.
2.) Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma haiweki uwazi wa kutangaza umiliki wa
mali za viongozi. Hii inapelekea viongozi kutoweka wazi mali wanazomiliki na ni
rahisi mtu kuzushiwa umiliki usio wa ukweli. Ni vyema Sekretarieti wakafanya
utafiti wa umiliki wa mali kwa viongozi wa Umma na kuweka taarifa hizo katika
tovuti ya Sekretariati ili kuwawezesha wananchi kuweza kuona mali zinazomilikiwa
na viongozi wao; na pale ambapo kiongozi hatakuwa ametoa taarifa ya umiliki huo
basi taarifa hiyo itolewe kwa Tume.
3.) Kwa kuwa leseni za udereva za sasa zinaweza kuweka kumbukumbu za makosa ya
usalama barabarani, basi TRA ikishirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani
zihakikishe ya kuwa Askari wa Usalama Barabarani wanatumia utaratibu huu wa
kisasa wa kutoa “notification” na kutoa risiti za malipo za elektroniki.
4.) Maduhuli ya Serikali sasa yakusanywe kwa kutumia risiti za elektroniki.
Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma yaanze kutumia risiti za
eletroniki mara moja ili kudhibiti upotevu wa mapato ya serikali yanayotokea hivi
sasa katika kutumia risiti zinazoandikwa kwa mkono. Pia ofisi za serikali zifanye
manunuzi yake kwa wafanyabiashara wanaotumia mashine za kielektroniki.
5.) “The Proceeds of Crime Act, 1991” ifanyiwe marekebisho na kuweka kifungu
kinachomwezesha AG/DPP kuwa na mamlaka ya kuomba mahakama kufungua kesi ya madai
(Civil Forfeiture) kwa watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi.