Rais Kikwete kujenga masoko mahususi ya bidhaa


Rais Jakaya Kikwete

Na Joachim mushi

SERIKALI imesema itahakikisha kabla ya kuondoka madarakani inajenga maeneo maalumu na masoko mahususi ya bidhaa mbalimbali ili kuwarahisishia wajasiria mali kupata soko la bidhaa hizo muda wote, tofauti na kutegemea maonesho ya Saba Saba pekee.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Rais Jakaya Kikwete alipokuwa akizungumza na wanahabari ndani ya Maonesho ya 35 ya Biashara Kimataifa katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam baada ya kumaliza ziara ya kutembelea mabanda mbalimbali katika maonesho hayo.

Rais Kikwete alisema kitendo cha wafanyabiashara kutegemea kuonesha bidhaa zao ama kuuza kipindi cha maonesho ya Saba Saba, hakitoshi hivyo Serikali inafanya utaratibu wa kujenga masoko mahususi ili wafanyabiashara wa bidhaa fulani wawe wakionesha na kuuza bidhaa hizo maeneo maalumu.

“Hili jambo lazima tulifanye maana hata wenzetu huko nje katika nchi mbalimbali wanafanya, ukienda utakuta kuna soko maalumu la bidhaa za batiki tu…na kwingine waweza kukuta soko maalumu la vitenge tu, pale utawakuta wajasiriamali wote wa vitenge wakionesha na kuuza bidhaa zao, na sisi lazima tufanye hivyo tuwe na masoko maalumu ya mwaka mzima,” alisema Rais Kikwete.

Alisema utaratibu huo utawasaidia wajasiriamali kupata masoko ya kudumu katika maeneo hayo hivyo kuwaongezea kipato tofauti na ilivyo sasa. Alisema nia ya Serikali ni kuhakikisha uchumi unakuwa kiujumla kwa kushirikisha sekta zote muhimu nchini.

Alisema si jambo jema Serikali kuanza kuzuia bidhaa za nje zinazoingia kwa utaratibu mzuri wala kampuni za nje kufanya shughuli zao ili kukuza zile za ndani, kwani hata kampuni za ndani nyingi bado ni changa ukilinganisha na zile za kutoka nje.

Aliongeza kuwa hata hivyo kuingia kwa kampuni hizo pamoja na bidhaa zao kunaleta changamoto na kutoa elimu ya kampuni na wafanyabiashara wa ndani kujifunza mbinu mbalimbali za kibiashara kutoka nje hivyo nao kunufaika kwa njia hiyo.

Aidha alibainisha kuwa kwa sasa Serikali inafanya tathmini za fedha ambazo ilizitoa kukopeshwa kwa wananchi ‘maarufu kama mabilioni ya JK’ kabla ya kutoa kiasi kingine kwa utaratibu ili wananchi wengi waendelee kunufaika na mikopo hiyo.

“Kuongeza fedha hizo za mikopo, tutaziongeza lakini kwa sasa bado tunafanya tathmini juu ya zile zilizotoka na baada ya hapo Serikali itaangalia iongeze kiasi gani maana hata zile zilizotolewa bado hazijaisha kabisa,” alisema Rais Kikwete akitoa ufafanuzu juu ya kuwawezesha wajasiriamali.

Akizungumzia suala la umeme, Rais Kikwete alisema matatizo ya umeme yanatokana na ukame ambao umekuwa ukitokea kwenye vyanzo vya umeme vinavyotegemea maji, jambo ambalo linaipa ugumu Serikali. Aliongeza inachokifanya Serikali ni kuhakikisha inapata vyanzo mbadala tofauti na umeme wa nguvu za maji ili nchi isiwe ikitegemea vyanzo vya aina moja.

Alisema japokuwa kwa sasa serikali imeagiza mitambo ya kufua umeme kutoka nje, vijekusaidia hali iliyopo hivi sasa, tatizo la umeme litakuwa limealizika kabisa baada ya miaka miwili kulingana na mipango iliyowekwa na Serikali.