Waziri Dk. Mwakyembe Afumua Mtandao wa ‘Unga’

Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe akizungumza na waandishi wa habari


WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe jana ameanika majina ya watu saba waliohusika kupitisha mabegi tisa yaliyokuwa na kilo 180 za dawa za kulevya zenye thamani ya Sh8 bilioni, Julai 5 mwaka huu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), wakiwamo maofisa usalama wanne wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na polisi mmoja.

Alisema mizigo ikishaondoka mikononi mwa abiria hukaguliwa tena kwa kutumia mbwa wa Idara ya Usalama wa Taifa, lakini siku ya tukio hilo mbwa hao walichelewa na walitumika baada ya mizigo kuingizwa kwenye masanduku ya chuma.

“Kwa abiria watatu kuwa na mabegi makubwa tisa yanayofanana si kitu cha kawaida kukwepa jicho la maofisa wa ushuru wa forodha na vyombo vya usalama, sijui walikuwa wapi siku hiyo?” alihoji Mwakyembe.

Juzi waziri huyo aliahidi kuyaweka hadharani majina ya watu wanaosafirisha dawa za kulevya nchini, na alitekeleza ahadi hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari, kusema kuwa watu hao wamenaswa baada ya mfumo wa kamera (CCTV) za uwanja huo kudaka matukio kadhaa yaliyotokea siku ya tukio hilo, kuanzia saa 9:25 hadi saa 10:30 alfajiri.

Ameagiza wafanyakazi hao wanne pamoja na askari polisi mwenye cheo cha koplo, mbeba mizigo na mfanyabiashara aliyekuwa na wasichana wawili waliokamatwa Afrika Kusini, (ambao hatuwezi kuwataja kutokana na kushindwa kuwapata kujieleza) kuchukuliwa hatua za kinidhamu, kukamatwa na kuunganishwa na watuhumiwa waliokwenda na mzigo huo Afrika Kusini.

Mabegi hayo yaliyokuwa na dawa za kulevya aina ya ‘Crystal Methamphetamine’, yalipitishwa na wasichana wawili wasanii aliowataja kuwa ni Agnes Gerald ‘Masogange’ na Melisa Edward ambao walidakwa siku hiyohiyo katika Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo, Afrika Kusini na tayari wameshafikishwa mahakamani.

Juzi Dk Mwakyembe alifanya ziara JNIA kukagua utendaji kazi kwenye uwanja huo ikiwa ni siku tatu baada ya ahadi aliyotoa akiwa Mwanza kwamba katika kipindi cha wiki mbili, atahakikisha anawakamata vigogo wote walio katika mtandao wa usafirishaji na uingizaji wa dawa za kulevya kupitia viwanja vyote vya ndege nchini.

Saa nane baada ya ziara hiyo, Maofisa wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege wanadaiwa kumkamata Edwin Monyo akiwa na kete 86 za dawa aina ya heroini na misokoto 34 ya bangi aliyokuwa akiisafirisha kwenda Italia kupitia Zurich.

Mpango ulivyosukwaHatua za wizara
Alisema wizara imeagiza TAA kuwa, kuanzia sasa mtu yeyote anayekamatwa na dawa za kulevya lazima apigwe picha na zisambazwe kwenye vyombo vya habari.

Pia ameliagiza Jeshi la Polisi kushirikiana na Polisi wa Kimataifa (Interpol) kumkamata mfanyabiashara anayedaiwa kuwasaidia Masogange na mwenzake kusafirisha dawa za kulevya ambaye alitoweka na mabegi matatu ya dawa hizo huko Afrika Kusini, “Akamatwe na kuunganishwa na kesi inayowakabili Watanzania hao wawili.”

Alisema mbeba mizigo anatakiwa kufukuzwa kazi na mwajiri wake na asiruhusiwe kukanyaga JNIA, kwamba serikali imewaagiza polisi kumkamata mtu huyo kwa lengo la kuunganishwa na wenzake kujibu mashtaka ya jinai chini ya sheria ya kuzuia dawa za kulevya, sura ya 95 ya mwaka 1996.

Alisema TAA inatakiwa kuwafukuza kazi mara moja wafanyakazi wake wanne waliohusika katika mpango huo, kuwakamata na kuwaunganisha katika mashtaka yanayowakabili.

“Jeshi la polisi limeagizwa kumwondoa mara moja askari mwenye cheo cha koplo anayedaiwa kuhusika katika tukio hilo na kumchukulia hatua za kinidhamu kwa kushiriki kwake kwa njia moja au nyingine kwenye njama za kupitisha mabegi hayo ya dawa za kulevya,” alisema.

Alifafanua kuwa Idara ya Usalama wa Taifa imeagizwa kuendesha uchunguzi wa kina kwa maofisa wake waliokuwa zamu siku ya tukio kwa kuchelewa kuwafikisha mbwa wakati mwafaka, jambo ambalo limeliletea taifa fedheha kubwa.

“Serikali imeziagiza taasisi zote zilizopo chini ya JNIA kutekeleza majukumu ipasavyo na kwa mujibu wa sheria na taratibu ili kuhakikisha dawa za kulevya hazipiti kwenye kiwanja hicho kikuu cha ndege nchini,” alisisitiza.

CHANZO: www.mwananchi.co.tz