CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewafukuza madiwani wake nane wa chama hicho mkoani Kagera, baada ya kutangaza kuwavua hadhi ya uwanachama wa chama hicho.
Kwa mujibu wa taarifa ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera iliyokutana 13/08/2013 imeamua kufikia uamuzi huo kwa mujibu wa utaratibu wa kutoa adhabu kwa viongozi wa CCM walio kwenye vyombo vya dola hasa wabunge na madiwani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape M. Nnauye alisema uamuzi huo umefikiwa mjini Bukoba baada ya kikao cha Halmashauri Kuu CCM mkoa wa Kagera.
Hata hivyo uamuzi wa kufukuzwa kwa viongozi hao unangoja Baraka za kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ndipo utekelezwe, ambacho kitakutana hivi karibuni mwezi huu.
“Hivyo basi, mpaka sasa Madiwani hao wanane waliosimamishwa wanapaswa kuendelea na kazi zao kama kawaida wakisubiri kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa kitakachoketi tarehe 23 Agosti, 2013 mjini Dodoma ambacho pamoja na mambo mengine kitapitia uamuzi huo wa Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Kagera.”
“Pamoja na hilo, tumepokea barua za Madiwani hao za kukata rufaa kupinga uamuzi huo wa Halmashauri Kuu ya Mkoa kwa msingi wa madai ya kukiukwa kwa utaratibu katika kufikia uamuzi huo.”
Hata hivyo katika taarifa hiyo CCM imewataka wananchi wa Bukoba na Kata husika, wanachama na viongozi wote kuwa watulivu katika kipindi hiki ambapo suala hili linashughulikiwa na vikao vya Kitaifa wa chama.
Taarifa zaidi ambazo mtandao huu umezipata zinadai madiwani hao wamejikuta katika kadhia hiyo baada kusaini hati ya kutaka kumng’oa madarakani Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani ambaye anakabiliwa na tuhuma kadhaa madarakani. Madiwani waliofukuzwa ni Richard Gaspar (Miembeni), Murungi Kichwabuta (CCM), Alexander Ngalinda (Buhembe) ambaye pia ni Naibu Meya, Yusuf Ngaiza (Kashai) ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa wilaya, Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe), Samwel Ruhangisa (Kitendagulo) na Dauda Kalumuna (Ijuganyondo).