POLISI mjini Zanzibar wameanza uchunguzi na kuwatafuta wanaume wawili ambao wanatuhumiwa kuwamwagia maji ya acid wanawake wawili raia wa Uingereza wakiwa matembezini mjini. Taarifa kutoka polisi mjini hapa zinasema wanawake hao walimwagiwa maji ya Acid katika nyuso zao baada ya kuvamiwa majira ya usiku.
Naibu Kamishna wa polisi mjini Zanzibar, alisema wanaume wawili waliwatendea wanawake hao kitendo hicho walipokuwa wakitembea katika barabara za mji wa kihistoria wa zanzibar. Wanawake hao inasemekana wanafanyia kazi shirika moja la kujitolea, hata hivyo nia ya shambulizi hilo haijajulikani hadi sasa.
Wakati huo huo, Rais wa Marekani, Barack Obama ameahidi kuisaidia Serikali ya Kenya katika kukarabati uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) baada ya kuungua moto eneo la kuwasili wageni wa ndege za kimataifa.
Katika ujumbe wake wa simu, Obama alisisitiza kuwa Marekani iko tayari kuisadia Kenya katika hali ile yoyote kutokana na ushikiano wake na Kenya. Obama pia aliwapa pole familia zilizowapoteza wapendwa wao katika mashambulizi ya bomu ya Agosti 1998 mjini Nairobi.
Hata hivyo, ndege za kimataifa zimeanza kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa jijini Nairobi JKIA, siku moja tu baada ya kitengo cha kuwasili wageni kuchomwa na moto mkubwa. Ndege ya kwanza ya kimataifa kuwasili katika uwanja huo ni ile iliotoka Uingereza na baadaye nyingine kutoka Tanzania na Bangkok zikawasili.
Manmo Jumatano, moto mkubwa uliotokea majira ya asubuhi, uliharibu kitengo cha kuwasilia wageni wa kimataifa. Vikundi vya wachunguzi viliwasili katika uwanja huo kufanya uchunguzi wao kubaini kilichosababisha moto huo. Abiria walikwama kutokana na mkasa huo ingawa waliweza kuondolewa nje ya uwanja kwa ajili ya usalama wao huku baadhi wakiangalia mizigo yao ikiteketea wasijue la kufanya.
Rais Uhuru Kenyatta aliwasili katika uwanja huo na kujionea uharibifu uliotokea na kiisha kutoa taarifa yake kupitia kwa msemaji wake Esipisu aliyesema kuwa chanzo cha moto huo kinachunguzwa.