CCM Yawagalagaza Wapinzani Uongozi wa Halmashauri Kibondo

Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Abdulrahman Kinana

Na Mwandishi Wetu, Kibondo

KATIKA hali inayothibitisha ule usemi wa mwanamuziki Chamilion wa Uganda kuwa “fitina yako bahati yangu” wapinzani wameanguka baada ya kushindwa vibaya kwenye uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeibuka mshindi kwenye nafasi zote za uongozi za kuiongoza Halmashauri hiyo, ushindi ambao umewaacha midomi wazi wapinzani waliokuwa wakisubiri kufaidi kwenye ugomvi wa madiwani wa CCM wilayani hapo.

Hii imetokea baada ya Diwani wa CCM Ndugu, Emily Msanya kuibuka mshindi kwa nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri baada ya kupata kura 14 kati ya 17 zilizopigwa na Makamu Mwenyekiti ni Apronary Mazinda ambaye pia alishinda kwa kura 14 kati ya 17.

Kuchaguliwa kwa madiwani hao na ushindi huo wa CCM kwenye ngome ya upinzani ambapo Mbunge wa jimbo hilo ni Ndg. Mkosamali wa NCCR-Mageuzi ni uthibitisho dhahiri kuwa CCM ina mkakati mkubwa wa kuzidhibiti ngome zote za upinzani nchini kuelekea uchaguzi wa 2014 na 2015.

Kabla ya uchaguzi huo palikuwa na mgogoro mkubwa kati ya madiwani wa CCM, mgogoro ambao ulitatuliwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi Ndg. Nape Nnauye kufuatia ziara yake ya kimyakimya ya siku moja wilayani Kibondo ambapo alikutana na madiwani hao wa CCM kwa zaidi ya masaa manne.

Matokeo haya ni kinyume kabisa na kile kilichoandikwa na Gazeti la Tanzania Daima la Agosti 7,2013 kuwa ‘ WIKI NGUMU KWA CCM” wakieleza kuwa CCM wangepoteza uchaguzi huu. Fitina hiyo ya TanzaniaDaima imegeuka kuwa bahati kwa CCM maana imetembeza kichapo cha haja kwenye uchaguzi huo.

Nape akiongea juu ya ushindi huo akinukuliwa na redio moja ya Mjini Mwanza alisema “ushindi huo ni mawingu mvua zenyewe zinakuja. Unajua hawa jamaa wanawekeza kwenye migogoro ndani ya CCM ili ikitokea hatukuelewana mahali basi wanazamia, hapa nimewazidi akili” alikaririwa Nape.