Moto ‘Wateketeza’ Uwanja wa Ndege wa Kenya

Baadhi ya sehemu za Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Jomo Kenyatta ukiwaka moto

UWANJA wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta umefungwa kwa muda baada ya moto mkubwa kutokea katika uwanja huo mjini Nairobi. Kwa sasa moto huo unaendelea kudhibitiwa na vyombo husika. Rais wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta amewasili katika uwanja huo na anatarajiwa kuhutubia waandishi wa habari baadaye. Hadi kufikia sasa hakuna ripoti zozote za majeruhi zimetokea kufuatia tukio la moto huo.

Taarifa zaidi zinasema kuwa kulikuwa na moshi mkubwa uliotoka katika eneo la kuondokea na kuingilia wageni. Mamlaka ya uwanja huo imesema kuwa tayari watu waliokuwa katika eneo hilo wameondolewa kwa usalama wao.

Taarifa zaidi zinasema shughuli ndani ya uwanja huo zimesimama huku safari zote za ndege zikiwa zimekatizwa na ndege zinazoingia katika uwanja huo zikielekezwa kutua katika viwanja vingine vya ndege kama vile Entebe, Dar es Salam, Kigali, Mombasa na kwingineko nchini Kenya.

Baadhi ya safari za ndege kutoka uwanja huo pia zimeahirishwa. Mwishoni mwa wiki jana baadhi ya wenye maduka ya Duty Free katika uwanja huo walifurushwa baada ya serikali kusema kuwa leseni za wenye maduka zilikuwa zimepitwa na muda. Hata hivyo chanzo cha moto bado hakijabainika.

CHANZO: BBC