CCM Yasema Inaimani na Tume ya Mabadiliko ya Katiba

Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari, katika Ukumbi wa Sekretarieti, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam. (Picha na Bashir Nkoromo).

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema bado kina imani na Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini, katika mchakato unaoendelea wa kupata katiba mpya. Imesema licha ya CCM kutofautiana kimawazo katika baadhi ya maeneo katika rasimu ya kwanza ya  katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, lakini haina ugomvi na tume hiyo.

Hayo yamesemwa na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Sekretarieti, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam.

“Tunawaheshimu sana wajumbe wa tume hii, na kwa kweli tunamatumaini nao sana kuwa watatimiza wajibu wao kwa weledi mkubwa”, alisema Nape.

Nape alibainisha kwamba  pamoja na maeneo mengine ya rasimu ya kwanza ya katiba ,  CCM ina mawazo tofauti kwenye suala la Muundo wa Muungano ambapo wakati rasimu inapendekeza muundo wa serikali tatu, CCM yenyewe inapendekeza  serikali mbili.

“Kama mnavyoona katika hili, wakati tume inapendekeza muundo wa serikali tatu sisi CCM tunapendekeza muundo wa serikali mbili, lakini hii haitufanyi tuwapuuze au tugombane na wale wenye mawazo tofauti na yetu”, alisema Nape na kuongeza;

“Kumekuwepo na ripoti na makala kadhaa zinazojaribu kuonyesha kama vile kuna mvutano kati ya tume na CCM, au CCM na wengine wenye mawazo tofauti na CCM. Ukweli ni kuwa hali hiyo inayojaribu kujengwa kwa nguvu si ya kweli. Tuache hoja zishindane kwa hoja na nguvu ya hoja ndio iwe msingi wa ushindani”.

Nape alitaka ushindani uwe kwenye hoja bila kushutumiana ili jatimaye mawazo ya wengi yasikilizwe na kuzingatiwa.

Alisema, CCM inasisitiza kuwa itaheshimu mawazo ya Watanzania, kwani katiba inayotengenezwa ni ya watanzania wote bila ya kujali itikadi zao.

“Naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru wale wote wanaounga mkono baadhi ya hoja za CCM hasa hoja ya serikali mbili. Tumeshuhudia maoni ya wajumbe wengi wa  mabaraza na wananchi kwa ujumla wakiunga mkono mawazo haya ya CCM ya muundo wa muungano wa serikali mbili na hoja kadhaa zingine”, alisema Nape na kuongeza;

“CCM tunapenda kuwashukuru wote. Tujadili kwa kuvumiliana, tukipendana na kuheshimiana. Tanzania yenye neema tele inawezekana”.