Waziri Aipongeza APRM kwa Kusambaza Nakala za Katiba

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano katika Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM), Bw. Hassan Abbas akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Gregory Teu. Kiongozi huyo alitembelea Maonesho ya Nane Nane mjini Dodoma Ijumaa na kutembelea Banda la pamoja la Taasisi za Wizara ya Mambo ya Nje za APRM na AICC Arusha.(Picha zote na Mpigapisha Maalum) 

NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Gregory Teu ameupongeza Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) kwa kugawa nakala za rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano kwa Wananchi. Naibu Waziri aliyasema hayo mara baada ya kutembelea banda la APRM kwenye maonesho yanayoendelea ya Nane Nane mjini Dodoma. Akizungumza mara baada ya kupatiwa maelezo kuhusu kazi zinazofanywa na taasisi za Wizara ya Mambo ya Nje zinazoshiriki Maonesho hayo za APRM Tanzania na AICC Arusha, Waziri huyo aliguswa baada ya kupatiwa nakala hiyo.

“Ni kazi nzui mnayoifanya hapa kama mnasaidia kugawa nakala hizi ili wananchi waweze kusoma na kufahamu kilichomo,” alisema Naibu Waziri Teu.

Tangu yalipoanza maonesho hayo APRM Tanzania imekuwa ikigawa bure rasimu za Katiba kwa lengo la kuwapatia wananchi wengi fursa ya kusoma na kufahamu kilichomo katika rasimu hiyo ya kwa kwanza.

Akitoa maelezo kwa Naibu Waziri Teu, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa APRM Tanzania, Bw. Hassan Abbas alisema APRM ilipokea nakala za kutosha kutoka Tume ya Marekebisho ya Katiba na imekuwa ikisaidia juhudi za Tume kuisambaza rasimu hiyo kwa wadau mbalimbali wa masuala ya utawala bora.

“Wananchi wengi waliofika hapa wamefurahi kupata nakala za rasimu. Wengi wamekiri kuwa hawakuwahi kuisoma au hata kufikiria kuwa ipo siku moja wataisoma nakala hiyo ya kwanza,” alisema Bw. Abbas.

Kutokana na umuhimu wa rasimu na masuala ya Katiba Naibu Waziri Teu aliishauri APRM kutenga dawati maalum ili kuwaelimisha zaidi wananchi kuhusu Rasimu hiyo na masuala ya Katiba.

Nao wananchi mbalimbali waliohudhuria na kupata nakala hizo wameeleza kufurahishwa kwao na uamuzi wa Serikali kuruhusu maoni juu ya Katiba mpya. “Sjawahi katika maisha yangu kushiriki zoezi muhimu kama hili,” alisema mkazi wa Dodoma aliyejitambulisha kwa jina la Joseph Augustine na kuongeza:

“Serikali ihakikishe basi wananchi wote wanapata hii katiba mpya itakapokamilika kuliko ilivyokuwa kwa ile ya zamani (ya sasa) ambayo mimi hadi sasa sijabahatika kuiona.”