Na Isaac Mwangi, EANA-Arusha
SERIKALI katika nchi wanachama zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimeambiwa kuongeza kasi ya kuzungumzia faida ya mtangamano wa jumuiya hiyo. Wanachama wa EAC ni pamoja na Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi, Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) linaripoti.
Mkurugenzi wa Huduma za Jamii katika Wizara ya Afrika Mashariki, Biashra na Utalii wa Kenya, Agnes Sila, alisema hayo juzi alipoipokea timu inayokwenda kufanya utafiti kubaini uelewa wa raia kuhusu masuala ya mtangamano wa EAC.
Timu ya utafiti huo nchini Kenya inaongozwa na mtaalamu wa masuala ya Habari, Sukhdev Chhatbar, ambaye alisema nchi zote tano za EAC zinahusika katika utafiti huo wa kubaini uelewa wa wananchi juu ya ushirikiano wa kikanda.
Timu itakuwapo mwambao mwa pwani ya Mombasa kwa siku kadhaa kabla ya kurejea jijini Nairobi. Baada ya kukamilisha kazi hiyo Nairobi, timu itaendelea na ratiba yake mjini Eldoret kaskazini mwa Bonde la Ufa. Utafiti huo utalenga makundi makubwa manne wakiwemo wakulima, wafanyabiashara, wutumishi wa serikali na wanawake walioko katika biashara.
Chhatbar alifafanua kwamba makundi hayo manne yamelengwa kwa sababu ndiyo nguzo ya mwenendo mzima wa mtangamano huo wa kanda. Kundi kubwa la wana Afrika Mashariki wamo ndani ya makundi hayo manne.
Utafiti huo unafanyika kwa njia ya madodoso, yanayopatikana katika lugha tatu za Kiingereza, Kiswahili na Kifaransa. Madodoso hayo yanatafuta kubaini uelewa na kiwango cha ufahamu kuhusu masuala ya EAC katika mtangamano kwa ujumla wake. Katika ngazi ya taifa, Sila alisema Kenya inafanya juhudi kuhamasisha raia wake juu ya masuala ya mwenendo wa mtangamano. Alisema juhudi hizo zinajumuisha kubaini changamoto zinazokabili mtangamano wa EAC.
Utafiti huo ulioanza Julai 16 utahitimishwa Agosti 27, mwaka huu. Timu hiyo imeshamaliza zoezi hiyo Uganda na Burundi. Utafiti huo umeandaliwa na EAC na kufadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Misaada la Ujerumani (GIZ).