Rais Kikwete Azindua Wilaya ya Kyerwa
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Julai 27, 2013, amezindua rasmi Wilaya Mpya ya Kyerwa katika Mkoa wa Kagera. Katika sherehe iliyofanyika katika eneo la Nkwenda na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi wa Kyerwa, Rais Kikwete ameambiwa kuwa Wilaya hiyo imeanzishwa miaka mwili kufuatia ahadi ya Mheshimiwa Rais mwenyewe ambayo aliitoa wilayani Karagwe alipotembelea wilaya hiyo Juni mwaka 2010.
Wilaya hiyo iliyokuwa sehemu ya Wilaya ya Karagwe ina jumla ya tarafa nne, kata 18 na vijiji 84 na watu 321,026 na ilipata Mkuu wake wa kwanza wa Wilaya mwaka jana, Mei 9, 2012.
Wilaya hiyo ambayo makao yake makuu yatakuwa katika eneo la Rubwera tayari Halmashauri yake ilikwishaidhinishwa na Waziri Mkuu tokea Novemba 23 mwaka 2013 inatarajiwa kupata Baraza la Madiwani mwezi ujao Agosti Mosi, mwaka huu, baada ya kuvunjwa kwa Baraza la Madiwani la Wilaya ya Karagwe wiki ijayo, Julai 31, ili kuruhusu uchaguzi mpya wa madiwani wa wilaya hizo mbili.
Wilaya ya Kyerwa inatarajiwa kuwa na madiwani 23 ikiwa ni pamoja na madiwani 18 wa kuchaguliwa kutoka katika kata zote 18 za Wilaya hiyo. Kwenye mkutano huo, Rais ameielekeza Wizara ya Ujenzi kuanza maandalizi ya kuijenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Bugene, Karagwe kupitia Wilaya ya Kyerwa hadi Mulongo kwenye mpaka wa Tanzania na Rwanda. Rais Kikwete amezindua Wilaya hiyo ikiwa ni sehemu ya shughuli za ziara yake ya siku sita katika Mkoa wa Kagera.