Mtoto Afichua Siri ya Polisi Kuua Baba Yake

Kamanda wa Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova

*Familia yachachamaa yataka uchunguzi huru

KUNDI la polisi wasiojulikana kwa mara nyingine wameendelea kulipaka matope jeshi hilo baada ya kutajwa kuhusika katika mauaji mengine ya raia wakati akiwa katika mikono yao. Tukio hilo jipya na la aina yake limefichuliwa na mtoto wa marehemu ambaye alisema, kabla ya kufikwa na mauti baba yake, alikamatwa na kupigwa na polisi katika maeneo ya Kurasini jijini Dar es Salaam.

Taarifa za polisi kuhusika na mauaji ya mwananchi huyo aliyetajwa kwa jina la Selemani Mwinyimsanga mwenye umri wa kati ya miaka 35 na 40 zilitolewa kwa mara ya kwanza na mtoto wa marehemu ambaye alishuhudia askari hao wakimpa kipigo baba yake. Kuvuja kwa taarifa hizo za polisi kuhusishwa na tukio hilo, kulielezwa jana na binamu wa marehemu, Joachim Mgembe wakati alipozungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam.

Akisimulia mkasa huo uliotokea Jumanne ya wiki iliyopita, Mgembe alimkariri mtoto huyo wa marehemu ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu aliyemtaja kwa jina moja la Geoffrey akisema aliona namna baba yake alivyokuwa amedhoofika baada ya kipigo hicho.

“Nilipata taarifa juzi kutoka kwa mtoto wa kaka wa marehemu anayeitwa,Nasoro Hamadi, kuwa baba yake mdogo ambaye ni marehemu, amefariki dunia.

“Alinieleza kuwa, Selemani alikamatwa na polisi katika eneo ambalo halikufahamika na kisha askari hao wakamchukua na kumpeleka nyumbani kwake Kurasini.

“Walipomfikisha nyumbani kwake, walianza kupekua ndani na inaonekana hawakukuta kitu.

“Baada ya upekuzi huo, wakaanza kumpiga, inasemekana walimpiga sana hadi akadhoofika na kwa bahati nzuri wakati wanampiga marehemu, alikuwapo mtoto wa mke wake anayeitwa,.

Mgembe alimkariri mtoto huyo akisema mara baada ya kipigo hicho polisi hao waliondoka na baba yake na wakaenda naye eneo lisilojulikana.

Alisema mara tu baada ya tukio hilo, kijana huyo alimpigia simu mama yake akimueleza kuhusu kile kilichotokea. Mawasiliano hayo yalisababisha mke huyo wa marehemu kurejea nyumbani kwa dharura na kutoa taarifa kwa ndugu na jamaa zake kabla ya kuanza kumtafuta mumewe katika vituo mbalimbali ya polisi.

Kwa mujibu wa Mgembe, polisi hao walimchukua marehemu hadi kituo cha polisi cha Oysterbay ambako inadaiwa marehemu akiwa hapo kabla mauti kumfika aliwasiliana kwa simu na dada yake kwa njia ya simu akimueleza namna alivyopigwa na polisi kwa kiwango cha kuhitaji msaada wa matibabu.

“Ndugu walikwenda pale Polisi Oysterbay ili kumdhamini lakini walipofika kituoni hapo, waliambiwa hakukuwa na taarifa za ndugu yetu na wakawashauri waende Kituo cha Polisi, Stakishari Ukonga ambako ndiko walikohisi marehemu angeweza kukutwa.

“Ndugu zangu hawakukata tamaa, walikwenda Stakishari, ambako nako hawakuambulia kitu zaidi ya kupewa majibu kuwa hawajamkamata mtu wa namna hiyo.

Baada ya majibu hayo, Mgembe alisema majibu hayo yalisababisha ndugu hao kurejea tena Polisi Oysterbay ambako ndugu yao aliwaeleza awali kwamba ndiko alikokuwa akishikiliwa. Wakiwa kituoni hapo, Mgembe anasema ndipo baadhi ya askari polisi wawili ambao hawakuweza kuwataja walipowaeleza kwamba ndugu yao waliyekuwa wakimtafuta alipoteza maisha kutokana na kipigo.

“Walipokuwa kituoni hapo, waliibiwa siri na askari wawili waliokutana nao kwenye ngazi na kuambiwa kuwa, ndugu yetu alifikishwa kituoni hapo, lakini kutokana na kipigo alichokuwa amepata, alikuwa amefariki dunia.

Mgembe alisema taarifa hizo zilisababisha dada wa marehemu kuangua kilio hapo hapo, tukio lililosababisha polisi waliofichua siri hiyo kutoweka, pengine kwa kuhofia usalama wao wa kikazi baada ya kufichua siri hiyo.

Baada ya taarifa hizo, ndugu wa marehemu walianza kuzunguka katika hospitali mbalimbali kumtafuta ndugu yao, wakianzia na Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako hawakufanikiwa. Baada ya kutoka hapo, walikwenda katika hospitali ya Mwananyamala, ambako walikuta mwili wa marehemu ndugu yao.

Akizungumzia tukio hilo, kaka mwingine wa marehemu, Hassan Mwinyimsanga alitaka uchunguzi ufanywe kuhusu mazingira tatanishi ya kifo cha ndugu yake. Gazeti hili lilipowasiliana na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alisema hakuwa na taarifa zozote za kuwapo kwa tukio la namna hiyo na akaahidi kulifuatilia.

Majibu hayo ya RPC Wambura yalisababisha gazeti hili kuwasiliana na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova ambaye naye alishindwa kueleza lolote kutokana na kuwa likizo. Badala yake, Kamanda Kova alilitaka gazeti hili kuwasiliana na viongozi wengine wa jeshi hilo.

CHANZO: www.mtanzania.co.tz