Mama Salma Kikwete Awataka Viongozi wa Dini Kuhubiri Amani

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akitoa nasaha zake baada kuwafuturisha viongozi wa serikali, madhehebu ya dini wa wilaya ya Mkuranga na wananchi wa kijiji cha Hoyoyo kilichoko karibu na Mkuranga katika Mkoa wa Pwani Julai 23, 2013. 

Na Anna Nkinda  – Maelezo

VIONGOZI wa dini nchini wametakiwa kuhubiri amani katika majukwaa yao ili jamii ielewe umuhimu wa kuwepo kwa amani na kuendelea kuishi kwa upendo na ushirikiano. Wito huo umetolewa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiwafuturisha wanakijiji cha Hoyoyo wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.

Mama Kikwete alisema kuwa viongozi wa dini wanajukumu kubwa la kuhakikisha kuwa waumini wao wanaelewa umuhimu wa amani katika nchi kwa kujenga mshikamano kama waasisi wa Tanzania walivyouanzisha.

“Katika shughuli yetu hii tumekusanyika watu wa dini mbalimbali wanaofunga mwezi huu na wengine mwezi mwingine lakini dua ni dua kupitia kwa mwanadamu yeyote Mwenyezi Mungu inamfikia, hivyo basi tuzidi kushikamana kwa kila jambo”.

Aliendelea kusema kuwa amani inatafutwa kwa miaka mingi lakini inaweza kutoweka kwa muda mchache hivyo basi kila mtu hasa viongozi wa dini watumie muda wao kuhubiri umuhimu wa amani katika nchi na neno amani lisitoweke  ndani ya vinywa vyao.

Kwa upande wake Sheikhe Athuman Kinyozi alimshukuru Mama Kikwete kwa futari aliyoiandaa kwa ajili yao na kusema kuwa mtu anayejitoa kwa ajili ya kufuturisha wengine  anapata thawabu kwa Mwenyezi Mungu.

Sheikhe Kinyozi alisema kuwa kufanya kitendo cha kufuturisha si lazima uwe na uwezo mkubwa kifedha bali unaweza ukanunua hata tende au maji na kuwapa watu waliofunga kile ulichowapa kikiwa ni kitu cha kwanza kutia midomoni mwao utalipwa thawabu za funga ya wale wote uliowapa kitu walichokula.