RAIS wa Sudan Kusini, Salva Kiir, amelivunja Baraza lake la Mawaziri pamoja na kumfukuza kazi, Makamu wa Rais Riak Machar katika mabadiliko makubwa zaidi kuwahi kutekelezwa katika historia ya miaka miwili ya taifa la hilo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na aliyekuwa Waziri wa Habari, Barnaba Marial Benjamin, ameliambia Shirika la Habari la BBC kuwa mawaziri wote kutoka upande wa Makamu wa Rais Riek Machar wameondolewa. Habari zaidi kutoka Sudan Kusini zinabainisha kuwa haijabainika iwapo kuna waziri yeyote miongoni mwa wale waliofutwa kazi atarejeshwa katika baraza jipya la mawaziri litakaloundwa upya na rais huyo.
Hata hivyo hakuna sababu iliyotolewa kuhusiana na hatua ya rais kuwafuta kazi maofisa hao wa ngazi za juu Serikalini, lakini wadadisi wanasema kuwa Rais Kiir na makamu wake Machar wamekuwa na mgogoro wa mamlaka kwa miezi kadhaa sasa huenda hali hiyo imechangia.
Sudan Kusini imekumbwa na matatizo chungu nzima hasa ya kiuchumi tangu kujitenga na Sudan mwaka 2011. Uthabiti wake umetatizwa na malumbano kati yake na Sudan kuhusu mipaka na swala la mafuta. Hivi karibuni baadhi ya maofisa wa Bwana Kiir, wamekuwa wakizungumzia kuwepo minong’ono kuhusu uongozi wake.
Ripoti zinasema kuwa Kiir anajitahidi kusalia na ushawishi katika chama cha Sudan People’s Liberation Movement (SPLM), ambacho kimeunda Serikali. Kwa upande wake Machar, ambaye mwezi Aprili alipunguziwa mamlaka, alisema huenda akagombea uongozi wa chama cha SPLM dhidi ya Rais Kiir, kabla ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2015.
-BBC