Waasi M23 wadaiwa Kubada na Kuuwa DRC

Baadhi ya waasi wa kundi la M23

SHIRIKA la kutetea haki za Binadamu la ‘Human Rights Watch’ limesema kuwa kundi la wapiganaji la M23 Mashariki mwa Jamhuri ya Demokrsia ya Congo limewaua zaidi ya watu 40 na kuwabaka zaidi ya wanawake na wasichana 60 tangu Machi mwaka huu.

Taarifa hizo zimepatikana baada ya shirika hilo kuwahoji zaidi ya watu 100 eneo hilo. Shirika hilo limesema licha ya vitendo hivyo viovu waasi hao wanalalamikiwa kwa kuwasajili kwa nguvu vijana huko DRC na wengine kutoka nchi jirani ya Rwanda kujiunga na kundi lao.

Kundi hilo limeongeza kuwa Jeshi la Rwanda bado linawasadia moja kwa moja waasi hao licha ya serikali ya Kigali kupinga hilo mara kwa mara. Wakati huo huo, jeshi la DRC limeshambulia ngome za waasi hao karibu na Mji wa Goma Mashariki mwa DRC.

Haya yalikuwa mashambulizi ya kwanza tangu vita kati ya pande hizo mbili kuanza Jumatatu asubuhi na kusitishwa siku hiyo mchana. Kundi hilo limesema liko umbali wa kilomita nne kutoka Mji wa Goma, ingawa limesema lengo lake ni kulazimisha Serikali kufanya mazungumzo nao wala sio kuteka Mji wa Goma.

M23 liliuteka Mji wa Goma, kwa siku kumi mwezi Novemba kabla ya kuondoka mjini humo kufuatia shinikizo za jamii ya kimataifa kufanya mazungumzo na Serikali ya Rais Joseph Kabila. Mazungumzo na Serikali yalianza mjini Kampala mwezi Disemba ingawa baada ya miezi miwili jeshi likaanza tena mapigano na waasi hao mwezi Julai 14.

Kulingana na taarifa za Umoja wa Mataifa inakadiriwa mapigano hayo yamesababisha takriban watu 4,200 kutoroka makwao.

-BBC