Mbunge Chadema aitaka Serikali kutaja mshahara kima cha chini

Na Mwandishi wa Thehabari Dodoma


Mbunge wa Viti Maalumu CHADEMA, Rose Kamili

MBUNGE wa Viti Maalumu CHADEMA, Rose Kamili ameitaka Serikali kueleza kinagaubaga kima cha chini cha mishahara kimepanda kwa kiasi gani na si kutoa maelezo ya jumla.

Kamili alitoa hiyo Bungeni jana wakati akichangia hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, ya Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2011/2012 iliyosoma juzi na Waziri Hawa Ghasia.

Alisema si jambo la busara kwa Serikali kutoa maelezo ya jumla kuhusu kupanda kwa mishahara kwani hiyo ni kiini macho kwa Watanzania ambao walikuwa wanasubiri kwa hamu kubwa kusikia kiwango kipya cha mishahara.

Mbunge huyo akiendelea kuzungumza alisema watumishi wa Tanzania hawana uhakika wa maisha yao kutokana na kiwango kidogo cha mishahara wanachopata, lakini jambo la kushangaza serikali imeshindwa kutoa tamko ili umma ujue mshahara umepanda kwa kiasi gani.

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), alisema haungi mkono hoja hiyo kwasababu watumishi wa umma wamepewa ahadi hewa.

“Naomba nianze kwa kuseme hivi sitaunga mkono hoja iliyopo, kwani jana baada ya bajeti hiyo kusomwa nimepigiwa simu na watu wengi sana wakiwemo wa jimboni kwangu wakitaka kujua mishahara imepanda kwa kiasi gani.

…Asilimia 40.2 iliyoelezwa na waziri ni hewa, nasema ni hewa kwasababu fedha hizo zimehusisha waajiriwa wapya, hivyo umma wa Watanzania wamedanganywa, hii si haki kuwa na ahadi hewa kama hizi,” alisema Mnyika.

Akiendelea kuzungumza Mnyika alisema Serikali tangu imeingia madarakani miezi saba iliyopita haijaleta matumaini kwa wananchi wake na kwamba taifa lipo kwenye hali mbaya kutokana na uzembe wa serikali.

Mnyika pia alimtaka Rais Jakaya Kikwete kuisafisha Ikulu kwa kuwaondoa watu wanaomshauri vibaya, na kuongeza kuwa “Rais alilitangazia taifa kuwa ifikapo Julai umeme wa megawatt 260 zitaanza kuzalishwa lakini leo ni Julai tupo katika mgawo wa umeme na mgawo mkubwa unakuja”

Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msingwa (CHADEMA), akichangia makadirio hayo alisema Idara ya Usalama wa Taifa haifanyi kazi yake ipasavyo jambo linalosababisha nchi iendelee kuibiwa rasilimali zake.

Alisema Idara hiyo inafanya kazi ya kudhibiti Vyama vya Siasa na kuacha mambo muhimu yakiharibika, hivyo akaitaka iende nje ikajifunze mbinu za kukuza uchumi wa nchi.

“Mimi nashangaa sana kuona Usalama wa Taifa wakitumiwa na CCM kuvidhibiti vyama vya CUF, NCCR- Mageuzi na CHADEMA, huku rasilimali za taifa hili zikiibiwa, misitu yetu inaibiwa, Twiga amepandishwa ndege na wanyama 126 wamesafirishwa, wao wanakuwa wapi?

…Taifa hili halina mwelekeo, watu wanagombea ubunge wakiamini kuwa watakuwa mawaziri baada ya kuahidiwa, Mwalimu Nyerere alisimamia kile anachokizungumza,” alisema Msingwa.

Mbunge wa Kisarawe, Selemani Jafo (CCM), aliwataka baadhi ya wabunge kutotumia vinywa vyao vizuri hivyo waache kumtukana Rais Jakaya Kikwete kwamba anasafiri ovyo hovyo kwani anapokwenda nje haendi kwa manufaa yake binafsi bali ya umma.

“Kuna baadhi yetu hapa wanatumia vinywa vyao vibaya kumsema Rais kwamba anatumia madaraka vibaya kwa kwenda nje ya nchi kila mara, rais anaangaika kwa ajili ya watanzania, wenyewe tumeshuhudia jana (juzi) kule Kigoma akiwatumikia wananchi na si kwamba anafanya mambo yake binafsi,” alisema Jafo.