UMOJA wa mataifa umesema upo tayari kupeleka jeshi katika uwanja wa mapambano huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kukabiliana na waasi. Hatua hiyo inayotokana na malalamiko ya wananchi walio andamana mjini Goma wakilalamika. Waandamanaji hao walilalamikia kitendo cha walinzi wa amani kutowasaidia majeshi ya Serikali kukabiliana na vitendo vya waasi maeneo hayo.
Jeshi la Umoja wa Mataifa (UN) nchini Congo limeonekana kujiweka kando wakati wapiganaji waasi wa kundi la M23 wanapofanya mashambulizi dhidi ya majeshi ya serikali katika eneo kubwa la mashariki la Mji wa Goma.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Martin Nersirky amenukuliwa na shirika la habari la Ufaransa, AFP akisema jeshi la ulinzi wa amani nchini Congo, MONUSCO kwa wakati wote katika operesheni zake nchini humo halijajiingiza katika uhasama.
Msemaji huyo ameongeza kusema majeshi ya bado yapo katika hali ya tahadhari na kujitayarisha kujiingiza katika mapigano hayo, kwa kujumuisha jeshi jipya kwa lililopo nchini humo kwa hivi sasa kwa ajili ya kuleta ustawi. Amesema operesheni hiyo inaweza kuwaweka katika hali ya wasiwasi wakazi wa eneo hilo la mashariki ya Kongo, na hasa Goma.
Kwa mujibu wa AFP, tangu jana kumekuwa kimya katika eneo la Goma. Lakini kulikuwa na maandamano katika mji huo, ambapo baadhi ya wamelituhumu jeshi hilo la Umoja wa Matiafa kwa kutotoa ushirikiano wa kutosha kwa majeshi ya serikali ya Kongo.
Hadi sasa kuna wanajeshi 2,000 kutoka Afrika Kusini, kati ya 3,000 wanaounda jeshi hilo la UN. Idadi iliyobaki kati ya hao inatoka Tanzania na Malawi. Majeshi hayo yanafanya tu, doria na kwamba mpaka sasa hawajafanya shambulizi lolote pamoja na kuwa na mamlaka ya kufanya hivyo kama inavyoelekeza mamlaka waliopewa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.
Msemaji wa Umoja huo Nesirky alisema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amesikitishwa na uhasama mpya katika maeneo ya mji mkuu wa Kivu ya Kaskazini. Kiongozi huyo wa ametaka pande zote husika eneo hilo kufanya jitihada kudhibiti kuongezeka kwa mgogoro huo ambao utazidisha matatizo kwa wakazi.
Waasi wa M23 walifanya mashambulizi Jumapili iliyopita ambapo Jeshi la Congo lilisema kiasi ya watu 130, waliuwawa.
-DW