Serikali ya Tanzania Yawaomba Wananchi Kushiriki Ulinzi wa Rasilimali

Hifadhi ya Kilimanjaro


Na Hassan Silayo- MAELEZO

SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imewaomba wananchi kusaidia katika katika ulinzi wa rasilimali nchini. Hayo yamesemwa jana na Afisa Habari wa Wizara hiyo Bi. Yustina Mallya wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari leo Jijini Dar es salaam.

“Wizara inaomba sote tuitafakari na kuitekeleza dhana ya Jeshi la Polisi ya Ulinzi Shirikishi ni muhimu kila mwananchi mzalendo wa nchi hii ashiriki kikamilifu kudumisha amani na ulinzi wa nchi na rasilimali zake zote,”alisema Yustina.

Aidha Yustina alisema ulindaji wa rasilimali hizo hasa wanyama pori utasaidia kujenga na kuimarisha utalii wa nchi kutokana na zaidi ya asilimia 90 utalii unategemea wanyamapori na hivyo kuingizia nchi fedha za kigeni na pia kukuza uchumi.

“Kwa hapa nchini zaidi ya asilimia 90 ya utalii unategemea wanyama pori hivyo, watalii wengi huja kuwaona, kuwapiga picha na kuondoka wachache huja kuwawinda kisheria na kuchukua nyara. Wanyamapori ndio wamebeba utalii katika Tanzania na kwa maana hiyo ndio, kwa kiasi kikubwa, wamebeba uchumi wa nchi hii,” alisema Yustina.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Kuzuia Ujangili kutoka wizara hiyo Bw. John Muya aliwataka wananchi waliokatazwa kuishi maeneo ya njia za wanyama kutekeleza agizo hilo ili kuepuka uharibifu unaofanywa na wanyama hao kipindi cha uhamiaji.

“Napenda kutoa wito kwa wananchi kuondoka kwenye yale maeneo ambayo ni mapito ya wanyama pindi wanapohama kuondoka ili kuondoa usumbufu na uharibifu wa mali.” Alisema Muya.

Yustina aliwataka wananchi kuacha kuwatazama baadhi ya wanyama kama Fisi na Tembo kama kero kwa wananchi, badala yake tuwatazame wanyamapori kama benki kubwa na kama mkombozi wa nchi yetu kiuchumi.