TAKWIMU zinaonesha mabadiliko ya idadi ya wakazi vijijini kwenda mijini ni kubwa. Katika nchi ya Tanzania idadi ya watu waishio mjini wataipiku idadi ya watu waishio vijijini ifikapo mwaka 2030. Tanzania pia upatikanaji wa miundombinu ni hafifu kwa sekta zote, na hivyo ni vigumu kwenda sambamba na ongezeko la idadi ya watu.
Tanzania kama zilivyo nchi nyingi zinazoendelea, imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali za maendeleo ya miji zikiwemo; ongezeko la watu kwa kasi mijini; miundombinu isiyokidhi mahitaji ya uendeshaji wa miji; uwezo mdogo wa rasilimali kwa ajili ya kutoa huduma toshelevu za jamii na kupanuka kwa kasi kwa maeneo ya miji bila kuzingatia taratibu za Mipango miji na Usimamizi usiokidhi kasi ya maendeleo ya miji katika Halmashauri zetu
Hata hivyo jitihada zinazoendelea kufanyika nchini Tanzania katika miradi mbalimbali zitaleta ahueni ya tatizo linalofikiriwa kutokea, ikiwa ni pamoja na miradi ya TSCP, Mpango wa Kuimarisha Serikali za Mitaa Mijini (ULGSP) na hata mradi unaofanana na TSCP na ULGSP, mahususi kwa Jiji la Dar es Salaam, (Dar es Salaam Metropolitan Development Project – DMDP), ulio katika mchakato wa kujiandaa kwa utekelezaji wake.
Mradi wa uendelezaji Miji (TSCP) unaoendelea kutekelezwa katika Miji 7 nchini (Arusha, Dodoma,Tanga, Mbeya, Mwanza, Mtwara na Kigoma), umezaa matunda kwa mradi mwingine wa ULGSP. Hali hii ilielezwa rasmi na Waziri Mkuu, Mizengo K. Pinda (Mb.) wakati akizindua mradi huo wa ULGSP – 18 juni, Kuringe Hall – Moshi.
Akitoa pongezi zake kwa timu ya TSCP, alisema kuwa mafanikio yaliyoonekana katika mradi wa TSCP yamerahisisha kupatikana kwa mkopo mwingine kutoka Banki ya Dunia kwa ajili ya kuendeleza azma hiyo hiyo, mradi huo umejikita katika kuimarisha Halmashauri za Miji 18, ambazo ni Miji yote iliyobaki ya Tanzania Bara, na mradi utagharimu kiasi cha Dola milioni 255 kwa kipindi cha miaka mitano.
Aidha Mhe. Pinda alieleza kuwa jambo muhimu sana la kuzingatiwa na kuhakikisha kuwa mradi huu unatekelezwa kwa kiasi cha watu kujidhihirishia wenyewe kwa kuona kwa vitendo mafanikio, alieleza kuwa Serikali haitafumbia macho uzembe au ubadhirifu wa fedha au vifaa utakaosababisha kazi hii kukwama au kutekelezwa chini ya kiwango.
Pia Mhe.Pinda alisisitizia Wananchi kushirikishwa kikamilifu, alisema; “Nasisitiza wadau wote washirikishwe katika ngazi zote na taarifa za utekelezaji wa mradi ziwekwe wazi ili wadau wote wajue, watoe maon ya kukosoa au kuboresha”. Aliendelea kusema; “Kwa wale wanasiasa wenzangu, ni fursa ya kufuatilia kwa karibu ili kuhakikisha mradi unafanikiwa kama tunavyotarajia”.
Aidha Mkurugenzi wa Benki ya Dunia – Tanzania, Bw. Philippe Dongier alieleza furaha yake ya kuona maendeleo mazuri ya utekelezaji wa TSCP, na kueleza kuwa ana matarajio makubwa zaidi na ULGSP. Alisema; “Lengo kuu la Mpango ni kujenga na kuimarisha uwezo wa Halmashauri kutoa huduma na usimamizi wa Miji. Kupitia mpango huu, mabadiliko ya ufanisi ya muda mrefu yanatarajiwa katika maeneo ya Mipango Miji, mfumo wa kudhibiti fedha, uwajibikaji, uendeshaji na matengenezo na ukusanyaji wa mapato,”.
Miji husika (18), imeshaandaa Mipango Mikakati tayari kwa kuanza utekelezaji ifikapo mwezi Julai 2013.Mradi umelenga kuendelea kuziimarisha Halmashauri za Miji katika maeneo makuu matano ili ziweze kutoa huduma bora zaidi kwa kuzingatia sera ya Ugatuaji Madaraka (D by D). Maeneo yaliyolengwa ni pamoja na; Uboreshaji wa mfumo wa Mipango miji, ukusanyaji wa mapato ya ndani hususan mapato yatokanayo na kodi ya majengo, uboreshaji wa mifumo ya udhibiti wa fedha, manunuzi na masuala ya mazingira na kijamii, uboreshaji wa mifumo ya utekelezaji, uendeshaji na utunzaji wa miundombinu kwa ajili ya huduma za jamii, na kuboresha uwajibikaji na uwazi. Na baadhi ya shughuli husika zitahusisha; ujenzi wa barabara, masoko, maeneo ya kupumzika na kudhibiti taka ngumu.
ULGSP ni mradi wa kwanza katika Bara la Afrika chini ya “Mpango kwa Matokeo” (Program for Results – P for R). “Mpango kwa Matokeo” ni mbinu ya utoaji fedha kulingana na matokeo ya utekelezaji malengo mliyojipangia. Chini ya Mpango huu, Halmashauri husika zitafanyiwa tathmini ya utekelezaji wa vigezo vilivyopangwa kila mwaka na fedha zitatolewa baada ya matokeo kuhakikiwa.
Mbali na mradi wa TSCP na ULGSP, Serikali ya Tanzania ikishirikiana na Benki ya Dunia na Wadau wengine kuanzia miaka ya 1990 imetekeleza Miradi ya Ukarabati wa Miundombinu Mijini [Urban Sector Rehabilitation Project (USRP)] kuanzia 1997 hadi 2004 kwa gharama ya dola za Kimarekani million 104.9. Mradi huu ulitekelezwa katika miji 9 ya Tanga, Moshi, Arusha, Mwanza, Tabora, Morogoro, Mbeya, Iringa na Dar es Salaam na Mradi wa kuzisaidia Serikali za Mitaa zote (Local Government Support Project – LGSP) kuanzia 2004 hadi 2012 nao ulikuwa ni mkopo wa Benki ya Dunia kwa gharama ya dola za Kimarekani million 52.