Na Magreth Kinabo – Maelezo
MAKAMU wa Rais Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Kongamano la Uwekezaji katika mkoa wa Tabora litakalofanyika Ijumaa kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dares Salaam na Mkuu wa Wilaya wa Tabora Mjini Suleiman Kumchaya kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Tabora Fatuma Mwasa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kongamano hilo.
“Tunamkaribisha mtu yeyote aje kuwekeza Tabora kwa kuwa soko tayari lipo. Tunataka kupandisha hadhi ya Mkoa wa Tabora ili hali ya umasikini iondoke,” alisema Kumchaya.
Akizungumzia kuhusu hali ya mkoa huo, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Longino Kazimoto alisema ni mkubwa kuliko miko mingine hivyo wanataka uwe na maendeleo makubwa ndio maana wanawakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.
Kazimoto aliongeza kuwa mkoa huo una rasilimali za kutosha, ambazo ni misitu hekari 75,685 sawa na asilimia 44, ambapo asali inapatikana kwa wingi, mifugo ipatayo milioni 3.2, matunda, hivyo wawekezaji wanaweza kuanzisha viwanda vya kusindika.
Aidha alisema mkoa huo hivi sasa kwa mwaka unaingizia Serikali Pato la Taifa Sh. bilioni 1.2 na pato la mwananchi wa kawaida ni Sh. 560,783 kwa mwaka. Kazimoto alisema katika mkoa huo kuna vikundi 46 vya vijana ambavyo vimeandaliwa ili kuweza kufuga nyuki kisasa ili kuweza kupata asali ya kusafirisha nje ya nchi.