Dk. Shein apokea ripoti ya kura za maoni na Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar


Pichani Dk. Shein akipokea ripoti hiyo kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Khatib Mwinchande. Picha kwa hisani ya Ikulu Zanzibar.

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ametoa pongezi kwa juhudi kubwa zilizochukuliwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar kwa kuendesha uchaguzi mkuu uliopita pamoja na kura ya maoni kwa ustadi mkubwa.

Dk. Shein aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar pamoja na Wajumbe wa Sekterieti ya Tume hiyo, mara baada ya kukabidhiwa Ripoti ya Kura ya Maoni na Ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2010 na Mwenyekiti wa Tume hiyo Bwana Khatib Mwinchande.

Katika maelezo yake, Dk. Shein aliwaeleza Wajumbe hao kuwa ripoti hizo ni muhimu na amekabidhiwa wakati muwafaka na kuahidi kuzifanyia kazi.

Alisema kuwa juhudi zilizochukuliwa na Tume hiyo ni kubwa na zinazofaa kupongezwa na kuungwa mkono.
Akielezea kwa upande wa Kura ya Maoni, Dk. Shein alisema kuwa licha ya kuwa ni mara ya kwanza kufanyika hapa Zanzibar lakini ilifanyika kwa ufanisi mkubwa.

Aidha, Dk. Shein aliahidi kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazoikabili Tume hiyo ili iendelee kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa chini ya uongozi wa Wajumbe hao.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Tume hiyo kutokana na hatua na juhudi inazochukua katika mchakato mzima wa kuendeleza Tume hiyo ikiwa ni pamoja na kuzichambua na kuzipitia Sheria wanazozitumia kwa lengo la kuziimarisha zaidi ili Tume hiyo iendelee kufanya kazi zake vizuri.

Naye Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Khatib Mwinchande alitoa shukurani zake kwa Rais Dk. Shein kwa mashirikiano makubwa inayoyapata.

Akitoa maelezo kwa niaba ya Wajumbe wa Tume hiyo waliofika Ikulu mjini Zanzibar, Mwenyekiti huyo alieleza kuwa madhumuni makubwa ya ujio wao huo ni kumkabidhi Rais Ripoti hizo mbili.

Aidha, Mwenyekiti Mwinchande alitumia fursa hiyo kumueleza Mhe. Rais juu ya taratibu mbali mbali na mipango endelevu ya Tume hiyo.

Mbali ya Mwenyekiti huyo Wajumbe wengine waliofika Ikulu kukabidhi ripoti hizo ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo Bwana Said Bakari Jecha, Bwana Abdulrahman Rashid, Bi Mwanabaraka Rashid, Bwana Ayoub Bakari, Bwana Nassor Khamis, Kaimu Mkurugenzi Bwana Idrisa Haji na Mwanasheria wa Tume ya Uchaguzi Bwana Khamis Issa.