MIMBARI YA RAMADHANI: Mgeni Mwenye Heri na Fadhila Mbalimbali kwa Waislamu

Ramadhan Kareem

LEO ni siku ya nne tangu Waislamu nchini waungane na wenzao kote duniani kutimiza moja ya nguzo tano za Kiislamu, ambayo ni kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Ibada ya funga ni nguzo ya nne kwa Waislamu ambayo imeamrishwa kwa kila Mwislamu mwenye sifa ya kutekeleza kufanya hivyo huku ukitarajiwa ujira mkubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu (S.W).

Nguzo hii ni lazima kwa kila Mwislamu aliyebalehe na kuwa na akili timamu huku wale walio na sababu zinazokubalika kwa mujibu wa imani na sharia ya Kiislamu, wakitakiwa kutoa kiasi cha kibaba (vipimo vya chakula) kwa ajili ya kuwalisha maskini kwa muda wote wa Mfungo wa Ramadhani.

Mwenyezi Mungu (S.W) ameujalia kuwa mwezi wa rehema kwa viumbe, ikizingatiwa kuwa Mwezi huu ndio usiku wake mmoja ujulikanao kwa ‘Laila-tul Kadir’ ambao imeteremshwa ndani yake Qur-ani Tukufu kuwa ni muongozo kwa watu wote.

Mbali ya muongozo, hoja za wazi za uongofu na upambanuzi baina ya haki na batili, pia. Ramadhani ni mwezi ambao hufunguliwa ndani yake milango ya pepo na kufungwa milango ya moto.

Ni kwa kuuzingatia umuhimu na nafasi ya mwezi wa Ramadhani, ndipo Mtume akaitoa khutba yake tukufu, khutba ya kihistoria, khutba kongwe katika kuupokea na kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Katika kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani, kuna masharti mengi ambayo mja hutakiwa kuyatekeleza ili swaumu yake iweze kukubaliwa na Mwenyezi Mungu kwa lengo la kupata thawabu zaidi.

Swaumu au kufunga ni amri ya Mwenyezi Mungu kwa waumini wa dini ya Kiislamu kupitia kwa Mtume Muhammad (S.A.W). Amri hiyo ya Mwenyezi Mungu imetajwa katika aya ya 182 ya Sura ya Pili, Sura-tul-Baqarah, ndani ya kitabu kitukufu cha Qur-an.

Katika aya hii, Allah (SW) anawaambia Waislamu kupitia Mtume Muhammad (S.A.W) kuwa, “Enyi mlioamini, mmelazimishwa kufunga (swaumu) kama walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kuwa wacha Mungu.” (Qur-an 2:183).

Kwa mujibu wa aya hii, utagundua kuwa lengo kubwa kwa Waislamu kulazimishwa kutekeleza ibada hii ya funga ni kwa wao kuweza kufikia ngazi au daraja la ucha Mungu wa kikwelikweli. Kwa maana kwamba endapo mja ataitekeleza ibada hii kwa kufuata sharti zote kikamilifu, dhahiri kiwango chake cha imani kitapanda.

Lakini, katika aya inayofuata ya 184 ya sura hiyo hiyo, inabainisha idadi ya siku hizo za kufunga kuwa ni siku chache tu, kati ya 29 na 30. Pia inatoa udhuru kwa watu ambao hawawezi kutekeleza ibada hii kutokana na sababu mbalimbali kwa kuwafahamisha nini cha kufanya.

Mwezi mtukufu wa Ramadhan umegawanyika katika makundi matatu ambayo yana siku kumi kila moja, na kila kundi moja la kumi lina faida zake kwa mwenye kutimiza kile kilichoagizwa na Mwenyezi Mungu.

Kumi la kwanza linajulikana kwa jina la Rehma (rehema), la pili Magh-fira (kusamehewa madhambi) na lile la mwisho linaitwa kumi la kuachwa huru na moto. Katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani vitu vinavyopaswa kufanywa zaidi ni kuswali, kutoa zaka na matendo mengine ambayo kwa kiasi kikubwa humpwekesha Mwenyezi Mungu.

Katika mwezi huu, kila jema analofanya mja hulipwa zaidi kuliko ambavyo analipwa katika siku za kawaida, ndiyo maana watu hufurika kwa wingi katika nyumba za ibada.

Kumi la Rehma ndiyo tumelianza hivi karibuni, ambapo mja atakayetekeleza kwa usahihi atapata baraka kwa kila anachokifanya huku shetani akifungwa minyororo ili asiweze kuwarubuni watu.

Mtu mwenye kutimiza yale yanayotakiwa katika kumi hili, hupata thawabu nyingi pamoja na kujifungulia milango ya kuingia katika kumi la pili ambalo ni Magh-fira.

Wanazuoni na hadithi mbalimbali zinatanabaisha kuwa mtu mwenye kufanya ibada na kusoma kitabu kitukufu cha Qur-an katika mwezi huu, husamehewa dhambi zake zote alizozitenda huko nyuma. Kumi la mwisho ni la kuachwa huru na moto, ambapo waja ambao wametenda mema katika makumi yaliyotangulia, huondolewa adhabu zote zilizokuwa zikimkabili siku ya kiama.

Mja yeyote ambaye malaika wakimkuta akifanya ibada na kusoma Qur-an, huwa mwenye kupata daraja ya juu kwa Mwenyezi Mungu pamoja na kufunguliwa mambo yake mengi ambayo yalikuwa yamekwazika.

Kimsingi mwezi huu ni wa mchumo kwa mja, kwa kuwa kila jambo jema analolifanya hulipwa maradufu (thawabu) na kwa mwenye kufanya maasi hakika atakuwa ni mtu mwenye kula hasara mbele ya Mwenyezi Mungu na atakabiliwa na adhabu kubwa siku ya kiama.

Wanazuoni mbalimbali wa Kiislamu wanasema mwezi huu ni kama chuo cha mafunzo ambapo baada ya kumalizika, waumini wanapaswa wawe wameelimika na kubadilika ili wawe kama wamezaliwa upya kutokana na kutakasika na maovu.

Nakutakia funga njema ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Wabillah tawfiq.

0655 54 91 54 au abdallahkhamis2009@gmail.com

CHANZO: www.freemedia.co.tz