WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imetangaza majina ya wanafunzi watakaojiunga na kidato cha tano, huku zaidi ya nafasi 10,000 zikikosa wanafunzi kutokana na kufeli masomo yao. Matokeo hayo yalitangazwa jana na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Phillipo Mulugo, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Mulugo alitangaza nafasi hizo ikiwa ni siku kadhaa baada ya Serikali kuyafanyia marekebisho matokeo ya mtihani wa kidato cha nne, uliofanyika mwaka jana na matokeo yake kutangazwa mwanzoni mwa mwaka huu. Katika matokeo hayo, zaidi ya asilimia 60 ya wanafunzi waliofanya mtihani huo, walifeli kwa kupata daraja sifuri, jambo lililoifanya Serikali kufanya marekebisho hayo kwa kile kilichoelezwa kuwa, usahihishaji wa mitihani ulifanywa kwa kutumia mfumo mpya.
Wakati akitangaza matokeo hayo, Mulugo alisema nafasi zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya wanafunzi wa kujiunga kidato cha tano ni 43,757. Mbali na hayo, naibu waziri huyo alitangaza pia nafasi za waliochaguliwa kujiunga na vyuo vya ufundi mwaka 2013.
Kwa mujibu wa Mulugo, nafasi zilizobaki bila wanafunzi ni za masomo ya ‘art’ ambayo wanafunzi waliokuwa wakiyasoma, hawakufanya vizuri.
“Kwa kipindi cha mwaka 2013, kumekuwa na tofauti hasa kwa masomo ya sayansi ambapo kulikuwa na nafasi 18,564 za masomo hayo na kwa upande wa masomo ya art kulikuwa na nafasi 25,193.
“Katika masomo ya sayansi, nafasi zimejazwa zote lakini kwa upande wa masomo ya art, zimebaki nafasi zaidi ya 10,000.
“Kwa kuangalia uchaguzi kwa ujumla, wanafunzi wanaojiunga na kidato cha tano mwaka huu, nafasi ambazo zimejazwa ni 33,683, lakini zaidi ya nafasi 10,000 zimebaki bila wanafunzi.
“Kubwa ambalo limebainika katika uchaguzi wa mwaka huu, ni kwamba tulikuwa na nafasi za kutosha, lakini kutokana na ufaulu kuwa chini, watahiniwa wengine wameondokewa na sifa.
“Kwa mfano, mchepuo wa PCB kulikuwa na nafasi 6,188, lakini zilizopangiwa ni nafasi 6,400, wakati katika mchepuo wa HKL kulikuwa na nafasi 5,300 na zilizopangiwa ni nafasi 1,527 tu.
“Kwa kifupi, ni kwamba wanafunzi waliochaguliwa kuingia kidato cha tano jumla yao ni 33,683, wakiwemo wavulana 23,383 na wasichana 10,300,” alisema Mulugo.
Kwa mujibu wa Mulugo, idadi ya waliochaguliwa ni ongezeko la wanafunzi 2,824, sawa na asilimia 9.15, ikilinganishwa na wanafunzi 30,859 waliochaguliwa mwaka 2012. Mbali na hilo, alisema wasichana 5,038 wamepangiwa kusoma masomo ya sayansi, ambao ni sawa na asilimia 48.91, huku wanafunzi 5262, sawa na asilimia 51.09 wamepangwa kusoma masomo ya art.
“Kwa uwiano huu wa kijinsi, takwimu zinaonyesha wasichana waliochaguliwa ni wachache ikilinganishwa na wavulana na hali hii inaonyesha wasichana waliofaulu kwa ubora wa alama nzuri walikuwa wachache.”
Akizungumzia uchaguzi wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na vyuo vya ufundi na taasisi ya menejimenti ya maendeleo ya maji mwaka huu, alisema jumla ya wanafunzi 530, wakiwemo wavulana 416 na wasichana 114, wamechaguliwa kujiunga na vyuo hivyo.
Alisema pia kwamba, kati ya hao, wanafunzi wa kike waliochaguliwa kujiunga na vyuo hivyo wameongezeka kutoka 47 mwaka 2012 hadi 114 mwaka huu.
Kuripoti shule
Naibu Waziri Mulogo, alisema kutokana na mabadiliko ya muhula wa masomo, wanafunzi wote waliochaguliwa wanatakiwa kuripoti katika shule walizopangiwa kabla ya Julai 29, mwaka huu.
CHANZO: www.mtanzania.co.tz