Rungwe hajakata tamaa ya urais

Mgombea urais 2010 kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, Hashim Rungwe.

Imeandikwa na Magnus Mahenge; Tarehe: 27th June 2011

 
 
 
 
 

 
 

UKIZUNGUMZA na Hashim Rungwe (62),utabaini  wazi ni mtu aliyeshiba mang’amuzi, hekima busara.

Rungwe amebobea kwenye siasa, biashara na uelewa wa mambo. Katika kinyang’anyiro cha 2010, alikuwa miongoni mwa wagombea urais saba waliotaka kuingia Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam.

Rungwe alipeperusha bendera ya NCCR – Mageuzi, chama ambacho katika muhula uliotangulia uchaguzi huo hakikuwa na mbunge hata mmoja. Rungwe hakusikika sana kabla, kumbe ndio wale hawavumi, lakini wamo.

Lakini alijitokeza na kuibuka na kura nyingi akiwaacha nyuma wagombea wawili. Mwanasiasa huyo alikwenda kuwania nafasi hiyo akitoka kwenye fani ya biashara ndani na nje ya nchi. Pamoja na kazi hiyo, yeye ni Wakili mahiri katika Mahakama Kuu ya Tanzania.

Katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa mwaka huo, Jakaya Kikwete aliibuka mshindi, Rungwe alishika nafasi ya tano, akiachwa nyuma na aliyekuwa akitetea kiti chake, Rais Jakaya Kikwete wa CCM, Dk. Wilbrod Slaa (Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na Peter Mziray wa APPT-Maendeleo.

Kwanini anataka kuwania tena nafasi hiyo ya urais 2015? Kwa sababu chama kilichopo madarakani, hakina nia ya dhati kuwatoa Watanzania katika umasikini uliokithiri. Rungwe anaamini kuwa Serikali ya chama tawala ikidhamiria kuwapa nafasi Watanzania wanaweza kujikwamua kiuchumi na kimaendeleo.

Wanaweza kuzalisha, kuvumbua na kutengeneza bidhaa zinazotengenezwa nje ya nchi. Maisha haya waliyonayo, hawajawezeshwa, hawajapewa nafasi badala yake wamepewa wanaoitwa wawekezaji kumbe kadiri yake, hao ni wafanyabiashara ambao wapo hapa nchini wakichuma zaidi.

Wapo Watanzania ambao wangeweza kuwekeza, kwa sababu wana uchungu na nchi yao kuliko hao wanaoitwa wawekezaji. Wapo wafanyabiashara kama yeye ambao wangeweza kuwa viongozi wazuri katika wizara, sekta na idara za biashara nchini.

Wapo Watanzania ambao si wanachama wa CCM ambao ni maarufu, wana taaluma na uzoefu na wengeweza kuisaidia Serikali katika kujenga uchumi kuliko wawekezaji wa jamii.

Mfano kama nafasi kumi anazopewa Rais kuteua wabunge wa kuingia bungeni, angeweza kuchagua watu wataalamu, mfano Profesa Lipumba kuingia katika sekta ya uchumi, wangesaidia kusukuma mbele maendeleo ya nchi.

Hivyo, mtindo wa Serikali ya chama tawala kukumbatia, kutofungua milango kwa ajili ya wataalamu wengine, kunaonesha wazi haina nia ya dhati kuendeleza wananchi wake.

Rungwe anaamini kuwa wapo wafanyabiashara nchini, ambao kama wangeruhusiwa kuwekeza wangewekeza na kujenga viwanda, biashara, nishati na huduma nyingine kuliko hao wanaoitwa wawekezaji.

Serikali inatakiwa kutoa nafasi ya kutosha kwa sekta binafsi kushika usukani, mfano katika umeme, watu wanaweza kufua au kuzalisha umeme, maadamu waruhusiwe. Kama sekta binafsi haina uwezo ingekuwa wajibu wa Serikali kuipa mtaji au kukopesha, ili kuzalisha, kutengeneza na kuunda bidhaa na kutoza tozo.

Sekta binafsi inaweza kufanya maajabu katika kuwaondoa Watanzania kutoka kwenye kero za umasikini, ujinga na maradhi. Serikali iliyopo madarakani haijaamua kuwasaidia wananchi wake, kwa kuwaruhusu watu na sekta binafsi kwa ujumla kutoa mchango katika kujenga uchumi wake.

Mfano, tatizo la usafiri jijini Dar es Salaam si kubwa, na halihitaji kupanua barabara. Kilichotakiwa ni kupasua mfereji na kujenga reli pembeni ya barabara. Reli hiyo ingesafirisha watu sambamba na mabasi.

Miundombinu ingeweza kuongezwa ili kuondoa kero ya usafiri, wala si kuwaondoa wananchi katika makazi yao ya zamani, bali kuanzisha mipya mahali pengine, kwani ni kawaida wananchi kufuata huduma mahali zilipo. NCCR-Mageuzi inaamini kuwa jamii inahitaji maisha bora kwa kufaidi mapato ya nchi yake.

Maendeleo ya jamii yatapatikana kutokana na Taifa lake kusaidia jamii yake. Wananchi wa Tanzania wanatakiwa kuishi kwa uhuru na haki, katika ustawi wao katika umoja wao, kwa lengo la kuinuana.

Rungwe alieleza sera za chama hicho wakati wa kampeni, hata kama alifanya kampeni katika mikoa miwili tu Kigoma na Dar es Salaam. Katika kampeni hizo, aliahidi kuwa kama angekuwa rais basi angefanya kila anachoweza kuwainua wananchi kwa kutumia rasilimali za umma.

Kutokana na uhaba wa fedha, sera hizo hazikufika mbali, hivyo mkakati wa chama ni kuhakikisha sera hizo zinafika katika mikoa mbalimbali nchini. Kwa sasa, chama hicho kinapata ruzuku kutokana na kuwa na wabunge wake wanne kiliowapata mkoani Kigoma, ruzuku ni kidogo lakini inayosaidia kukiendesha chama.

Lengo la chama ni kuhakikisha kinapita kuwashawishi vijana wajiunge na chama hicho, ambao ndio wapigakura wa sasa. Hivyo chama kitakuwa katika kampeni za kunadi sera ni kuhakikisha vijana wengi wanajiunga na chama hicho ili kuwa mtaji katika uchaguzi 2010.

Rungwe yupo radhi kugombea tena 2015, kama chama kitampitisha. Atagombea tena hata kama atakuwa na umri wa miaka 66. Anasema umri huo ndio wa viongozi wengi wa Afrika, wanakuwa wamekomaa vizuri kisiasa.

Kupata wabunge wanne katika chama, kumechochea hamasa katika Bunge, hivyo akiteuliwa kupeperusha bendera ya chama atahakikisha wanapata wabunge wengi zaidi. Hata kama Bunge la sasa limejaa ubabe, na kuegemea chama tawala zaidi, jambo ambalo Rungwe anasema Spika wa Bunge angetakiwa awe mtu wa kuchaguliwa.

Ingetakiwa kutangaza nafasi na mtu mwenye sifa agombee apigiwe kura kuwa spika, badala ya utaratibu wa sasa wa spika kuwa mbunge wa chama. Sambamba na spika, magavana wa kuongoza mikoa, wapatikane kwa kuchaguliwa, kuliko wanaopewa nafasi hizo ambao si wa maeneo hayo.

Chama chake kinaamini kuwa, mtu wa kuchaguliwa anawajibika zaidi kwa watu kuliko wa kuteuliwa. NCCR-Mageuzi inajipanga kuongeza wanachama na wabunge ili siku moja rais wa nchi atoke chama hicho. Nani anajua kesho, labda lisemwalo lipo…

Source: HabariLeo