*Mandla amtuhumu Mbuso kuzaa na mkewe
CHIFU Zwelivelile Mandlesizwe Dilubhunga ‘Mandla’ Mandela (39), ambaye ni mjukuu mkubwa wa kiume wa Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, amemtuhumu mdogo wake, Mbuso Mandela (22) kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mkewe.
Tuhuma hizo nzito ndani ya familia ya Mandela, zimeibuliwa na Mandla kwa kumtaja jina moja kwa moja Mbuso kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mke wake wa pili, Anais Grimaud, ambaye alimpa ujauzito. Mandla na Mbuso ni watoto wa Marehemu Makgatho Mandela ambaye ni mtoto wa kiume wa Mandela kwa mkewe wa kwanza, Marehemu Evelyne Maso.
Watu walio karibu na familia ya Mandela, wamepata kukaririwa na vyombo vya habari vya nchini hapa wakieleza kuwa, Mandla amekuwa akilalamika mara nyingi kuwa mke wake ambaye wameshatalikiana, alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mmoja wa ndugu zake, lakini hakuwahi kumtaja kwa jina.
Katika malalamiko yake hayo, Mandla alikaririwa akieleza kuwa, ndugu yake alimpa mimba mke wake na kuzaa naye mtoto mmoja jambo ambalo wanafamilia wamelifumbia macho wakati wanajua alitendewa vibaya.
Alhamisi wiki iliyopita, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari huko Mvezo, Eastern Cape, baada ya kushindwa kesi aliyokuwa amefunguliwa na shangazi yake, Makaziwe Mandela ya kuvamia eneo la makaburi usiku na kuiba mabaki ya miili ya watoto watatu wa Mandela, Mandla alisema anashangazwa na watu wanaojiita wanafamilia ya Mandela kudai wanataka amani ndani ya ukoo wakati malalamiko yake hawajawahi kuyashughulikia.
Katika mkutano wake huo, Mandla alisema mke wake aliyemuita ni mzuri, Anais, ambaye ni raia wa Ufaransa, alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mdogo wake wa damu aliyemtaja jina kwa mara ya kwanza, kuwa ni Mbuso.
Alisema kwamba, alipopata taarifa hizo, alishtuka na kuumia na alimtaja mtoto ambaye mke wake alizaa na mdogo wake Mbuso kuwa anaitwa Nkosi Qheya II Zanethemba Mandela.
Mandla alisema alilazimika kuachana na mkewe huyo aliyemuoa mwaka 2010 na kwamba aliamua kumbadili jina mtoto aliyezaa na Mbuso na kumuita Nkosikazi Nobubule, kabla hajaondoka kwenye makazi ya Mandla na kurejea kwao Ufaransa.
Tuhuma hizi zilizotolewa na Mandla juzi kwa mara ya kwanza, ziliripotiwa na Gazeti la Sunday Sun la Afrika Kusini mwaka jana na kuibuka tena wiki iliyopita.
Taarifa hizo, zimezidi kuipa nguvu hofu ya baadhi ya watu wanaofuatilia mtafaruku wa ndani ya familia ya Mandela ambaye kwa sasa anapigania uhai akiwa hospitalini.
Kwa zaidi ya wiki mbili sasa, familia ya Mandela imekuwa katika mnyukano wa kugombea uhalali wa eneo linalostahili kuwa maalumu kwa ajili ya kuzika marehemu wa familia hiyo baada ya Mandla kuhamisha mabaki ya miili ya watoto watatu wa Mandela, waliokuwa wamezikwa katika nyumba yake iliyoko kijijini Qunu na kwenda kuwazika kwenye makazi yake ya kichifu ya Mzove.
Mahakama Kuu ya Mthatha ya Jimbo la Eastern Cape ilimtia hatiani Mandla aliyekuwa akishitakiwa na wanafamilia 16, ambapo ilimuamuru arejeshe mabaki ya miili hiyo Qunu.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa familia yake, Mandela bado yuko mahututi hospitali mjini Pretoria na hakuna taariza zozote za mabadiliko ya afya yake.
CHANZO: www.mtanzania.co.tz