Hotuba ya Rais Jakaya Kikwete Katika Tamsaha la Matumaini Jijini Dar es Salaam

Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete akihutubia katika Tamasha la Matumaini Uwanja wa Taifa

HOTUBA YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA UFUNGUZI WA TAMASHA LA MATUMAINI, UWANJA WA TAIFA DAR ES SALAAM, TAREHE 07 JULAI, 2013

Ndugu Wananchi;
Nakupongeza sana ndugu Erick Shigongo kwa kuandaa tamasha hili adhimu lenye mchanganyiko wa mambo mengi. Bahati nzuri mambo yote ni mazuri na yanayalifanyia taifa letu mambo mema. Sala ya pamoja kuliombea taifa, burudani mbalimbali zikiwemo za muziki, mchezo wa ngumi na mpira wa miguu.
Pengine faida kubwa zaidi ya Tamasha lenyewe hili ni kujenga moyo wa upendo, umoja, ushirikiano na moyo wa uzalendo miongoni mwa Watanzania wa marika yote: watoto, watu wazima na wazee. Miongoni mwa watu wa makabila yote, rangi zote, dini zote na miongoni mwa wafuasi wa vyama vyote vya siasa.
Katika kipindi hiki ambacho maadui wa umoja, amani na utulivu wa nchi yetu wanahangaika usiku na mchana kuleta mifarakano miongoni mwa Watanzania, matukio kama Tamsha hili ndilo jibu zuri kwao. Kupitia Tamasha kama hili tunawajibu kuwa Watanzania hatutaki, hatukubali na wala hatudanganyiki. Tuwapelekee ujumbe huo bila kumung’unya maneno kuwa njama zao zimeshindwa na kamwe hazitafanikiwa.
Lakini, tamasha hili pia lipeleke ujumbe kwa wanasiasa na wafuasi wao kuwa kutafuta umaarufu, kuungwa mkono au ushindi kwa kupandikiza chuki miongoni mwa Watanzania kwa misingi ya dini zao, rangi zao, na maeneo watokayo nako hakutawasaidia. Walishindwa wakoloni kwa sera yao ya wagawe uwatawale, hataweza mswahili. Isitoshe ni kutenda dhambi kubwa na kutowatendea haki Watanzania, Mungu wao, dini zao na vyama vyao vya siasa kuingiza dini katika siasa au siasa katika dini. Kiongozi wa siasa anayesema dini yetu ni hii au kiongozi wa dini anayesema Chama chetu ni hiki wote ni wababaishaji. Wanasema mambo ambayo hayana uhusiano wo wote na dini. Kiongozi wa dini huyo awe mkweli tu kwamba, ni mwanachama au mpenzi wa Chama cha siasa aliyeamua kutumia nafasi yake ya uongozi wa dini au uumini wake kuendeleza maslahi ya Chama chake. Hakuna lolote la dini hapo na wala hakuna kitabu kitakatifu cha dini yoyote kinachotaja Chama cha siasa cha kufuata.
Kiongozi wa siasa anayetumia dini kujenga Chama chake amefilisika hoja za kisiasa. Isitoshe Sheria ya Usajili wa Vyama iko wazi. Inazuia kutumia udini, ukabila na aina zote za ubaguzi. Watu hawa wamegubikwa na tamaa ya madaraka iliyovuka mipaka ya utu. Sijui kama watu hawa hawatambui athari zake. Tunaweza kufika siku makanisa na misikiti ikagawanyika kwa upenzi na ufuasi wa vyama vya siasa. Tutazikwaza dini zetu na nchi yetu kuiweka mahala pabaya.
Tuwaache wanasiasa na wanachama wagawanyike kwa vyama vyao wanavyovipenda lakini makanisa na misikiti pawe mahali pa kuwaunganisha. Mwenyezi Mungu awe ni muunganishaji wao. Lakini tukiendelea na mikakati ninayoiona na kuisikia inaendelea hata katika nyumba za ibada, viongozi wa dini watashindwa kuwaunganisha waumini wao. Badala ya watu kutambuana kama Waislaimu au Wakristo wataanza kujuana kwa vyama vya siasa. Ni hatari kubwa kwa dini kwani upenzi wa watu kwa vyama vya siasa ni vitu vinavyobadilika kulingana na sera, matukio na mazingira. Hivi tunataka na imani ya watu kwa dini iwe inabadilika na mazingira?
Tuyalinde mambo yanayotuunganisha ili yadumu. Tusiyaendekeze mambo yanayotugawa. Pale ambapo siasa zinagawanisha, dini, michezo na mengineyo yanayowaunganisha yatekelezwe kwani yanaweza kusaidia kupunguza uhasama na yanaweza kusaidia kuponya. Zitto Kabwe na William Ngeleja wako vyama viwili vinavyoshindana katika majukwaa ya siasa, lakini leo watacheza upande mmoja wa Wabunge wa Simba. Halima Mdee, Grace Kiwelu, Mohamed Misinga wao ni viongozi wa Yanga Bungeni. Mambo yanayotuunganisha tuyape kipaumbele kusisitiza umoja wetu, kujenga upendo na kupunguza makali ya tofauti zetu.
Ndugu Shigongo wa Global Publishers nakupongeza sana kwa kufanya jambo linaloponya jamii. Matukio kama haya yanatakiwa yawe mengi zaidi nchini kwani yana manufaa makubwa kwa nchi yetu na watu wake. Sisi katika Serikali tunaunga mkono. Yaendelezeni na yadumisheni.
Nakushukuru pia kwa uamuzi wako wa busara wa kutumia asilimia 20 ya pesa zinazokusanywa kusaidia ujenzi wa mabweni ya wasichana katika shule nane za sekondari katika mikoa ya Manyara, Tanga, Dodoma, Lindi, Ruvuma, Mara, Mwanza na Kigoma. Ni jambo jema sana. Asante sana.
Kwa ndugu zangu Wabunge, wasanii wa muziki na filamu na wanamichezo wengine waliojitolea kutuburudisha leo nawapongeza na kuwatakia kila heri. Tumekuja kuwashuhudia na kuburudika nanyi. Naomba mtuburudishe na kuwaonyesha vijana kuwa ujuzi hauzeeki.
Kwa mara nyingine nashukuru kualikwa.
Asanteni sana.