Lowassa Achangia Machinga Mwanza Shs Milioni 20

Edward Lowassa

WAZIRI Mkuu aliyejiuzuru, Edward Lowassa, ametoa Sh20 milioni kusaidia wafanyabiashara ndogondogo maarufu Machinga wa Mtaa wa Makoroboi, ili kuwajengea uwezo wa kukuza mitaji ya biashara zao. Akizungumza na Wamachinga hao, Lowassa alisema jukumu la kuwasaidia Machinga linapaswa kuwa la wafanyabiashara wote na kwamba, iwapo hawatasaidiwa hawatakuwa salama.

“Hamuwezi kuwa mnakimbizana nao Machinga kila uchao hawa, wawekeeni mazingira safi, wafanyabiashara mnayo sababu za kuwachangia, msipowachangia mjue watakula sahani moja nao,” alisema Lowassa.

Alisema Machinga lazima wachangiwe ili nao wafaidi matunda ya nchi na kwamba. jukumu la kuwachangia linapaswa kufanywa na wafanyabiashara wakubwa wa Mwanza.

“Wasaidie nao wale…tupishane kula wengine tutakula mkate na wao mhogo, lakini lazima wote wale,” alisema Lowassa.

Alisema kiwango alichochangia ni kama cha kusaidia Machinga wa Makoroboi, aliomba kuandaliwa kwa hafla kubwa kwa ajili ya kuchangia Sh1 bilioni kwa ajili ya Machinga wote Mwanza. Lowassa alisema jukumu la kuandaa hafla nyingine kupata Sh1 bilioni amelikabidhi kwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM, Dk Raphael Chegeni, Mbunge wa Kwimba, Shanif Mansoor, Mkurugenzi wa Nyanza Bottling Co. Ltd, Chrstopher Gachuma Artaf Mansoor ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Mafuta ya Moil.

“RPC ukitaka kukomesha wezi mjini kaa na machinga kuwasaidia, wanawajua wenzi hawa… wasaidieni maana mkiwasaidia mnatekeleza ilani ya CCM,” alisema.

CHANZO: http://www.mwananchi.co.tz