Mandela Aikoroga Afrika Kusini

Rais wa Afrika Kusini,Jacob Zuma (kulia) akiwa na mzee Nelson Mandela

*Mjukuu ataka Winnie, Graca wasiingilie ukoo
*Askofu Tutu, Zuma, Makamu wa Rais waingilia


SASA kuna dalili kuwa familia ya rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, imeparaganyika kutokana na ugomvi kuhusu eneo la makaburi. Mandla Mandela, mjukuu mkubwa wa kiume wa Mandela ambaye juzi alishindwa kesi aliyokuwa amefunguliwa na shangazi yake, Makaziwe Mandela, ya kuvamia eneo la makaburi ya ukoo lililoko Qunu na kuiba mabaki ya miili ya wanafamilia watatu aliyokwenda kuizika kwenye himaya yake ya Mzove, juzi alikutana na waandishi wa habari na kutoa tuhuma nzito dhidi ya ndugu zake.

Katika mkutano wake huo uliofanyikia Mzove, Eastern Cape, Mandla alisema amesikitishwa na kukatishwa tamaa na ndugu zake kutokana na kitendo chao cha kutanguliza tamaa ya kutaka kudhibiti utajiri alionao Mandela na kukiuka tamko lake la mahali alipoelekeza kuzikwa baada ya kufa kwake. Akiwa amefuatana na mama yake mzazi, mkewe na wanafamilia wengine wanaomuunga mkono, Mandla pia alimshambulia mdogo wake, Ndaba Mandela, kwa kutoa tuhuma nzito na mbaya kuhusu kuzaliwa kwake.

Mandla alisema alitamani baba yake mzazi angekuwapo wakati mdogo wake huyo akimshambulia kwa maneno hayo machafu.
Akirejea tuhuma ambazo Ndaba alizitoa dhidi yake, alisema mdogo wake huyo alivieleza vyombo vya habari kuwa yeye (Mandla) hafai kuongoza watu kwa sababu kuzaliwa kwake katika familia ya Makgatho Mandela kuna utata, kauli aliyoeleza kuwa inaichafua familia.

Hata hivyo, Mandla alisema hawezi kujiingiza katika vita chafu yenye lengo la kuibomoa familia ya Mandela mbele ya jamii. Akizungumzia hatua ya shangazi yake, Makaziwe, kumfungulia kesi mahakamani akiungwa mkono na Winnie ambaye ni mtalaka wa Mandela na Graca Machel, mke wa Mandela, alisema anawashangaa kwa sababu sasa kila mtu anataka kuonekana kuwa ni wa familia hiyo.

Mandla alisema shangazi yake Makaziwe ni mtoto wa nne wa Mandela kutoka kwa mke wa kwanza, marehemu Evelyne na alikwishaolewa na kuachika katika ndoa yake ya kwanza na baadaye aliolewa tena na mtu aliyemtaja kwa jina la Issac Amuah. Alisema Makaziwe ni mke wa Amuah hivyo anapaswa kujielekeza katika kushughulikia masuala ya familia ya mume wake huyo badala ya ukoo wa Mandela.

Pia aliwageukia bibi zake wa kufikia, Winnie na Graca ambao alieleza kuwa wao ni waolewaji katika familia hiyo hivyo hawapaswi kuingilia wala hawana kauli katika mambo ya utamaduni ya ukoo wa Mandela. Akizungumzia kile alichoeleza kuwa ni kiini cha ugomvi wa eneo la maalumu la kuzikia wanafamilia wa Mandela, alisema utajiri alionao babu yake ndiyo uliosababisha vurugu hizo.

Mandla alisema wote wanaopambana naye sasa wakitaka kuwa na haki ya kumiliki au kusimamia mazishi ya Mandela atakapokufa, wanavutwa kufanywa hivyo na ukwasi mkubwa ambao rais huyo mstaafu anao. Kauli ya Mandla ni mwendelezo wa vita ya wanaukoo wa Mandela ambayo iliibuka baada ya Makaziwe kurejee Afrika Kusini kumwangalia baba yake ambaye amelazwa katika hospitali ya Medi Clinic akisumbuliwa na ugonjwa wa mapafu.

Makaziwe na wafamilia wapatao 16, walimfungulia kesi mahakamani Mandla, wakimtaka arejeshe mabaki ya miili ya watoto watatu wa Mandela ambayo aliihaamisha kutoka katika makaburi ya ukoo yaliyoko Qunu, na kuyapeleka katika himaya yake ya Mzove ambako ni chifu. Mahakama Kuu ya Mthatha ya Eastern Cape iliyokuwa ikisikiliza shauri hilo, ilitoa hukumu iliyomtaka Mandla kurejesha miili hiyo huku ikieleza kuwa uamuzi wake wa kuhamisha mabaki ya miili hiyo haukubaliki.

CHANZO: http://www.mtanzania.co.tz