SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Burundi kuchezesha mechi ya kwanza ya mchujo ya Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Uganda (The Cranes) itakayofanyika Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Waamuzi hao ni Thierry Nkurunziza atakayepuliza filimbi wakati wasaidizi wake watakuwa Jean Claude Birumushahu na Pascal Ndimunzigo. Mwamuzi wa akiba (fourth official) ni pacifique Ndabihawenimana.
Kamishna wa mechi hiyo Gebreyesus Tesfaye kutoka Eritrea. Tesfaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Eritrea na mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Mashindano ya CHAN.
Fainali Airtel Rising Stars ‘Live’ SuperSport
Fainali za michuano ya Airtel Rising Stars kwa wavulana na wasichana zinazochezwa kesho (Julai 6 mwaka huu) Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam zitaoneshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha SuperSport.
Mechi za fainali ambazo mgeni rasmi atakuwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makala zitachezwa kuanzia saa 7.30 mchana kwa wasichana wakati ile ya wavulana itaanza saa 9.30 alasiri.
Nusu fainali za mashindano hayo ambazo pia zinaonekana moja kwa moja SuperSport zinachezwa leo (Julai 5 mwaka huu). Kwa upande wa wasichana ni kati ya timu za Kinondoni na Kigoma wakati Ilala inaumana na Temeke.
Kwa upande wa wavulana nusu fainali ya kwanza ni kati ya Mwanza na Ilala ambapo baadaye itafuatiwa na nyingine kati ya Morogoro na Kinondoni. Mechi za kutafuta mshindi wa tatu zitachezwa kesho asubuhi (Julai 6 mwaka huu).
28 KUSHIRIKI KOZI YA FIFA 11 FOR HEALTH
Jumla ya makocha wa mpira wa miguu na walimu 28 kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na shule za msingi na sekondari wameteuliwa kuhudhuria kozi ya FIFA 11 For Health inayoanza keshokutwa (Julai 7 mwaka huu) Homboro mkoani Dodoma.
Kozi hiyo itakayomalizika Julai 20 mwaka huu itakuwa chini ya ukufunzi wa Rogasian Kaijage ambaye pia ni Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars).
Washiriki ni Abdul Mikoroti (Shule ya Msingi Nzasa), Baltazar Kagimbo (Shule ya Msingi Tabata Jica), Baraka Baltazar (Shule ya Msingi Muhimbili), David Kivinge (Shule ya Msingi Temeke), Dismas Haonga (Tambaza Sekondari), Exuperus Kisaka (Shule ya Msingi Mavurunza) na Hadija Kambi (Shule ya Msingi Karume).
Hamis Chimgege (Shule ya Msingi Tusiime), Hobokela Kajigili (Shule ya Msingi Buguruni), Issack Mhanza (Shule ya Msingi Airwing), Job Ndugusa (Shule ya Msingi Upanga), John Sebabili (TFF), Lutta Rucharaba (Shule ya Msingi Montfort), Maua Rahidi (Shule ya Msingi Uhuru Wasichana), Michael Bundala (TFF) na Mussa Kapama (Shule ya Msingi Bunju ‘A’).
Priscus Silayo (Shule ya Msingi J.K. Nyerere), Peter Manyika (TFF), Rajabu Asserd (Shule ya Msingi Mtoni Kijichi), Raphael Matola (TFF), Raymond Rupia (St. Anne Maria Academy), Renatus Magolanga (Ulongoni Sekondari), Ruth Mahenge (Shule ya Msingi Chang’ombe), Said Pambaleo (TFF), Sebastian Nkoma (TFF), Titus Michael (TFF), Wane Mkisi (Jangwani Sekondari),
LIUNDA KUSIMAMIA MECHI YA CHAN
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua Leslie Liunda wa Tanzania kuwa Kamishna wa mechi kati ya Burundi na Sudan itakayochezwa jijini Bujumbura.
Mechi hiyo ya kwanza ya mchujo ya Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) itafanyika keshokutwa (Julai 7 mwaka huu). Liunda anatarajia kuondoka leo usiku (Julai 5 mwaka huu) kwenda Bujumbura.