Siku 27 za Mandela Akipigania Uhai Wake

Mzee Nelson Mandela

MAMBO yanayofanyika katika maeneo matatu ya Afrika Kusini, Hospitali ya Medclinic alikolazwa, katika makazi yake Mtaa wa Houghton, Barabara ya Laan 12, Johannesburg na makazi yake ya zamani huko Soweto, yanaashiria kwamba huenda lolote likatokea kuhusu afya ya Rais wake wa kwanza mzalendo, Nelson Mandela ambaye kwa siku ya 27 yupo hospitalini akiwa mahututi.

Baadhi ya wananchi wamekata tamaa kuhusu afya ya shujaa wao huyo na wanapofika nje ya Hospitali ya Medclinic, Pretoria alikolazwa, hushindwa kujizuia na kumwaga machozi. Baadhi yao wamekuwa wakisema ‘wako tayari kwa taarifa mbaya’ kuhusu kiongozi huyo aliyeongoza vita dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Mandela (94) ambaye sasa anatajwa kwa jina la Tata yaani Baba wa Taifa la Afrika Kusini, amelazwa katika hospitali hiyo ya magonjwa ya moyo na hali yake inaelezwa kuwa ni mbaya huku taarifa zikisema ‘anapumua kwa msaada wa mashine’.

Hali hiyo imewachanganya wananchi wa Afrika Kusini akiwamo Rais Jacob Zuma na familia ya Mandela ambayo tayari imeingia katika mgogoro mkubwa unaotafsiriwa na baadhi ya watu kwamba ni ‘kuwania madaraka’ ikiwa kiongozi huyo atafariki dunia.

Usiku wa kuamkia Jumamosi, Mwenyekiti wa Taifa wa Wanawake wa Chama tawala cha ANC, Baleka Mbete aliongoza maombi ya kumwombea Mandela kwa wanachama na makada wake waliopo katika Majimbo ya Cape Town na Eastern Cape huku akisisitiza: “Lazima wananchi wa Afrika Kusini wafike mahali wamruhusu Mandela ampumzike kwa mapenzi ya Mungu.”

Ukubwa kwa kishindo cha ugonjwa wa Mandela unaonekana hospitalini Medclinic alikolazwa, katika makazi yake Mtaa wa Houghton, Barabara ya Laan 12, Johannesburg na makazi yake ya zamani huko Soweto kwani maeneo hayo yamekuwa na harakati zisizokoma. Watu kwa mamia, wamekuwa wakifika wakiwa wamebeba mabango, kadi, mishumaa na maua, wengine katika makundi wakiimba, kusoma maneno ya Mungu na kufanya sala.

Wapo wanaoifananisha hali iliyopo nje ya kuta za Medclinic na Houghton na ukuta uliokuwa umezunguka jela alikokuwa amefungwa katika Kisiwa cha Robben kwa miaka 18 kati ya 27 aliyokaa gerezani.

“Kama watu walivyokuwa wakikaa nje ya kuta za Gereza la Robben na kupaza sauti zao kwamba wanataka Mandela aachiwe huru, ndivyo inavyoonekana leo. Watu wanapaza sauti, wanataka Mandela kutoka ndani ya kuta za Medclinic,” anasema mmoja wa watu waliokuwa kwenye lango la kuingia hospitalini hapo.

Kulia mwa lango hilo lililopo Mtaa wa Celliers, kuna idadi kubwa ya kadi na mabango ambavyo vina ujumbe mbalimbali kwa ajili ya Mandela, maua na mishumaa ambayo huwashwa na watu wanaofika sehemu hiyo. Kutokana na hali hiyo, mtaa huo umefungwa pande zote mbili kwa polisi kuweka vizuizi.

Jumamosi iliyopita, hofu juu ya afya ya Mandela iliongezeka hasa baada ya kuwapo kwa pilika nyingi Houghton zilizodumu kwa saa kadhaa, zikiwamo usafi usio wa kawaida uliojumuisha utengenezaji wa bustani za maua, ufagiaji wa barabara na matengenezo ya njia za umeme.

Mmoja wa majirani wa Mandela, Jacob Brews alisema harakati hizo si za kawaida na kwamba huenda ‘kuna jambo la ziada’.

Matukio hayo kwa jumla yake yamevivutia vyombo vya habari vya Afrika Kusini na vya kimataifa ambavyo vimeweka kambi katika maeneo hayo matatu yanayoonekana kuwa ni muhimu vikisubiri chochote kitakachotokea.

Vyombo hivyo viliingia katika mgogoro na polisi wa upande mmoja na familia ya Mandela kwa upande mwingine hasa kutokana na uwepo wake katika lango kuu la Medclinic.

Wiki iliyopita, polisi wa Pretoria waliwaamuru waandishi wa habari kuondoa magari na vifaa vyao nje ya hospitali hiyo kutokana na kile walichokiita ‘sababu za kiusalama,’ amri ambayo hata hivyo, haikutekelezwa.

Amri hiyo ya polisi ilitanguliwa na kauli ya binti mkubwa wa Mandela, Makaziwe ambaye alivikosoa vyombo vya habari kwamba vimeshindwa ‘kuheshimu desturi za Kiafrika pamoja na hisia za familia’ kuhusu ugonjwa wa baba yake.

Hata hivyo, kwa jinsi hali ilivyo, kauli za viongozi na harakati katika makazi yote ya Mandela, ni vigumu kwa wanahabari kukaa kimya katika tukio linalomgusa Mandela ambaye ni mtu maarufu ndani na nje ya Afrika Kusini.

Mgogoro wa ‘mazishi’ ya Mandela

Utata wa afya ya Mandela unachagizwa zaidi na hali ya sintofahamu inayoendelea ndani ya familia yake kiasi cha kuufikisha mahakamani mgogoro unaohusishwa na ‘mazishi yake.’

Familia inavutana juu ya ni wapi kiongozi huyo atazikwa lakini kwa sura ambayo inahusisha watoto wa Mandela ambao walifariki siku zilizopita na kuzikwa eneo la Qunu kabla ya baadaye mabaki ya miili yao kuhamishwa kinyemela kwenda eneo la Mvezo ambako ni makazi ya mjukuu mkubwa wa Mandela alitwaye Mandla.

Idadi kubwa ya wanafamilia wa Mandela wakiongozwa na binti mkubwa, Makaziwe (60), wanataka mzee wao huyo azikwe Qunu lakini upande mwingine ukiongozwa na Mandla (38) unataka azikwe Mvezo.

Hoja kubwa na swali ambalo baadhi ya watu wamekuwa wakiuliza ni kwamba ikiwa Mandela yuko hai ni kwa nini kuwepo mjadala wa mahali atakapozikwa?

Mkazi mmoja wa Johannesburg, Doroth Nyati alihoji: “Kama mtu hajafa mnawezaje kukaa kujadili mahali pa kumzika, ndiyo maana nimekwambia ni dhahiri kwamba Mzee Madiba (Mandela) tayari amefariki, ila wanatuficha tu.”

Jana, Mahakama Kuu ya Eastern Cape ilitoa uamuzi kwamba mabaki ya miili ya watoto hao yarejeshwe Qunu ifikapo saa tisa ya jana hiyohiyo ikimaanisha kwamba Mandla ambaye pia ni mbunge katika eneo hilo alishindwa kesi.

Amri hiyo ya Jaji Lusindiso Pakade inamaanisha kwamba marehemu hao sasa watazikwa kwa mara ya tatu; ya kwanza ni wakati walipofariki dunia kwa nyakati tofauti, pili miili yao ilipohamishwa kinyemela na Mandla kwenda Mvezo na tatu ni jana wakati wa utekelezaji wa amri ya mahakama.

Makaburi hayo ya Mandela ni ya mtoto wake kwa kwanza wa kike Makaziwe aliyefariki dunia akiwa mchanga 1948, mtoto wa pili wa Mandela, Madiba Thembekile aliyefariki katika ajali ya gari 1969 na baba yake Mandla aliyefariki 2005 kwa magonjwa yenye uhusiano na Ukimwi.

Mandla alihamisha makaburi hayo kwa siri mwaka 2011 ikiwa ni hatua ya kutaka babu yake; Mzee Mandela akifa naye azikwe Mvezo ili kuwavutia watalii katika kijiji hicho ambacho yeye ni kiongozi (chifu) wake.

Mandela aliwahi kunukuliwa akisema kwamba akifa angependa azikwe pembezoni mwa walipozikwa ndugu zake ambako ni Qunu, hivyo Mandla alihamisha makaburi hayo ikiwa ni hatua ya kushawishi kwamba babu yake huyo azikwe Mvezo ambako makaburi hayo yatakuwa.

Kutokana na hali hiyo, Makaziwe aliwaongoza wanafamilia kufungua kesi dhidi ya Mandla wakiomba Mahakama imwamuru kurejesha mabaki ya miili aliyoihamisha ‘bila ridhaa ya wanafamilia’.

Uamuzi wa mahakama ni pigo kwa Mandla ambaye pia anakabiliwa na hatari nyingine mbili; kwanza ni kuanza kwa mkakati wa kumvua madaraka ya uchifu wa Mvezo, lakini pili ni kufunguliwa kwa mashtaka ya jinai kwa kosa la kuchezea makaburi.

Ndugu wa kambo wa Mandla, Ndaba alikaririwa akisema viongozi wa kimila wanakusudia kuchukua hatua ya kumvua madaraka ndugu yake huyo kutokana na kukiuka miiko, mila za jadi kwa kuhamisha mabaki ya miili ya wanafamilia waliokuwa wamezikwa Qunu na kuizika upya Mvezo.

Wakati hayo yakiendelea, polisi wa Western Cape wamethibitisha kuanza uchunguzi wa tuhuma kwamba Mandla alichezea makaburi, hatua mbayo inamweka pabaya na kuzidisha mgogoro katika familia hiyo.

Afya kuzorota

Jumapili Juni 23, mwaka huu, Rais Zuma alitangaza kwamba afya ya Mandela ni mbaya taarifa ambayo ilizua sintofahamu, hofu na taharuki kwa wananchi wa Afrika Kusini.

Hofu hiyo ilizidi pale Rais Zuma alipoahirisha ziara yake ya kwenda Maputo Msumbiji, Juni 26 alikotakiwa kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kutokana na kile alichosema kuwa ni kutokana na afya ya Mandela.

Siku iliyofuata Juni 27, mwaka huu Zuma katika taarifa kupiti kwa msemaji wake, Mac Maharaj kwamba hali ya Mandela ina unafuu na kwamba bado yu mahututi lakini imara. Tangu wakati huo hadi leo Ikulu ya Pretoria imekuwa ikitoa taarifa kwamba hali ya kiongozi huyo haijabadilika hadi sasa. Taarifa rasmi zinasema Mandela anasumbuliwa na figo ambazo zimeshindwa kufanya kazi, lakini taarifa zaidi zinasema madaktari wamekuwa wakitibu zaidi magonjwa nyemelezi yanayotokana na ugonjwa wa msingi.

CHANZO/na kusoma zaidi: www.mwananchi.co.tz