EAC Yashiriki Tamasha la Filamu Zanzibar

Tamasha la Filamu Zanzibar-2013

Na Mtua Salira, EANA-Arusha

KWA mara ya kwanza katika historia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Sekretarieti ya jumuiya hiyo inashiriki katika Tamasha la Kimataifa la Filamu Zanzibar (ZIFF) kuongeza uelewa zaidi wa jumuia kwa watengenezaji wa filamu na wasanii juu ya masuala ya mtangamano.

Tamasha hilo la 16 litakalochukua wiki zima na ambalo ni moja ya matamasha makubwa kabisa Kusini mwa jangwa la Sahara, lilifunguliwa Jumapili na litaendelea hadi Julai 6.

EAC kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) limeandaa warsha ya uandishi wa skripti za filamu juu ya matangamano wa kikanda na kuwezeshwa na Mtengenezaji wa filamu na mwandishi wa skripti mashuhuri wa kutoka Nigeria, Femi Kayode.
Skripti itakayokuwa bora zaidi itatengezwa katika makala maalum.

Akifungua warsha hiyo Juzi, Mkuu wa Mawasiliano na Masuala ya Umma wa EAC, Richard Owora Othieno alisema Sekretarieti ina mpango wa kutengeneza makala maalum ya elimu huhusu mwenendo mzima wa EAC kwa lengo kuwafanya wana Afrika Mashariki kuwa na uelewa wa kutosha juu ya EAC.

“Tutatengeneza makala maalum yatakayoeleza kinagaubaga juu ya masuala ya mtangamano na kuongeza kasi juu ya ajenda ya uelewa zaidi kuhusu shughuli za EAC na mipango yake,” aliwaambia washiriki wa warsha hiyo.

Alifafanua kwamba hapo baadaye EAC itafanya maonyeha ya filamu juu ya mtangamano wa EAC katika tamasha hilo la ZIFF. Meneja wa GIZ anayeshughulikia Mtangamano wa EAC, Miriam Heidtmann alisema taasisi yake itaendelea kuunga mkono juhudi za ushirikiano wa jumuiya hiyo.

“Tuko tayari kuunga mkono mafunzo kwa waandishi wa habari na masuala yanayoendana nayo ili kuongeza uelewa wa wana Afrika Mashariki kuhusu EAC,” alisema.