RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amewashukuru wananchi kwa kushiriki kikamilifu na kufanikisha kwa kiwango cha juu kabisa matukio ya kitaifa ya karibuni ikiwamo ziara ya siku mbili ya Barack Obama, Rais wa Marekani na mkewe Mama Michelle Obama.
Matukio mengine yaliyofanyika nchini na ambayo yamepata mafanikio makubwa kwa sababu ya mchango na ushiriki mzuri wa wananchi ni pamoja na Mkutano wa Kimataifa wa Smart Partnership International Dialogue 2013 na Mkutano wa Wake wa Marais wa siku mbili ulioanza Julai 2, 2013 mjini Dar es Salaam.
Miongoni mwa wageni maarufu wanaoshiriki katika mkutano huo ni pamoja na Mheshimiwa George W. Bush, Rais wa zamani wa Marekani na mkewe Mama Laura Bush pamoja na wake wa marais wa Afrika Kusini, Ethiopia, Mozambique, Ghana, Sierra Leone na Uganda. Vile vile, Rais Kikwete amewashukuru viongozi na wasimamizi wote wa matukio na shughuli hizo kwa kutoa uongozi thabiti ambao hatimaye umewezesha matukio hayo kumalizika vizuri na malengo yaliyokusudiwa kufikiwa.
Aidha, Rais Kikwete amevishukuru vyombo vya habari vya hapa nchini kwa mchango wao mkubwa wa kuwahabarisha na kuwaelimisha wananchi kabla, wakati na baada ya matukio yenyewe kuwa yamemalizika kwa yale yaliyomalizika.
Pia, Rais Kikwete amezishukuru taasisi na vyombo vyote vya Serikali, vikiwamo vyombo vya ulinzi na usalama kwa kufanya kazi bila kuchoka ili kufanikisha shughuli hizo.
Rais pia amezishukuru taasisi za kibiashara na makampuni binafsi kwa mchango wao katika kufanikisha shughuli hizi akisisitiza kuwa ushiriki wa wafanyabiashara na taasisi za kibiashara katika shughuli hizo ni dalili njema kuwa ushirikiano wa sekta za umma na sekta binafsi umeanza kufanya kazi vizuri katika Tanzania.
“Napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru wananchi wote, na hasa wakazi wa Dar es Salaam, kwa mchango wenu mkubwa katika kufanikisha matukio haya muhimu ya kitaifa. Kwa pamoja tumeonyesha ukarimu wetu wa jadi kwa viongozi na wageni ambao wameshiriki katika matukio hayo.”
Rais amewaambia wananchi: “Tumeonyesha uvumilivu na utulivu mkubwa wakati wote wa matukio hayo. Natambua mazingira yanayojengeka tunapokuwa na ugeni mkubwa wa nje lakini bado tumeonyesha ukomavu wa hali ya juu kama taifa. Nawashukuru sana nyie wananchi kwa kufanikisha yote haya kwa sababu bila ushiriki wenu pengine matokeo ya shughuli hizo yangekuwa tofauti. Najivunia sana ushiriki wenu katika shughuli zote hizi za kitaifa. Mumeijengea nchi yetu heshima kubwa.”
Kwa viongozi na wasimamizi wa shughuli hizo, Rais Kikwete amesema: “Uongozi wenu umejidhihirisha waziwazi wakati wa matukio haya. Nawashukuruni nyote na hasa viongozi wa Dar es Salaam ambao walikuwa wenyeji wetu wakati wote wa shughuli hizi. Najua haikuwa kazi rahisi hata kidogo. Natambua kuwa wakati mwingine tulifanya kazi chini ya shinikizo kubwa lakini nawashukuru sana kwa kufanikisha haya yote.”
Kwa vyombo vya habari, Rais Kikwete amesema: “Nawashukuru wamiliki, wahariri na waandishi wa habari wa vyombo vyetu vya habari kwa mchango wenu wa kiwango cha juu katika kufanikisha yote haya. Asanteni sana. Ninaamini kuwa tutaendeleza uzoefu uliojengeka katika wiki moja ya matukio haya kwa manufaa ya nchi yetu na watu wetu.”