Na Mwandishi Maalum, Addis Ababa-Ethiopia
MAKAMU Wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohammed Gharib Bilal ameiwakilisha Tanzania katika Mkutano wa Umoja wa Afrika unaojadili namna ya kumaliza Baa la Njaa katika nchi za Afrika. Mkutano huo wa siku moja umefanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia Jumatatu Julai Mosi, 2013 ambapo nchi washiriki wamekumbusha kuhusu Azimio la Maputo walilolitoa miaka 10 iliyopita yaani mwaka 2003, azimio lililolenga kukabiliana na Njaa na Utapiamlo.
Azimio hilo lililenga kuzitaka nchi za Afrika kukabiliana na Baa la Njaa sambamba na kuhakikisha kuwa wananchi wa Bara hili, si tu kwamba wanapata uhakika wa chakula, bali kula chakula bora chenye virutubisho vinavyohitajika katika kulinda afya za binadamu na hivyo kuwa na uwezo wa kukabiliana na magonjwa. Pia azimio hilo lilizitaka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kuhakikisha zinatanua bajeti zake za Kilimo ili zifikia asilimia 10 ya Bajeti Kuu na pia kukifanya Kilimo kuchangia kwa asimilia 6 katika ukuaji wa uchumi wa nchi za Afrika.
Katika mkutano huo, Makamu wa Rais alieleza kuwa Tanzania inashirikiana bega kwa bega na nchi za Afrika katika kuhakikisha kuwa Bara hili linakabiliana vilivyo na baa la njaa na hivyo kutokomeza Baa hilo kama nchi hizo zilivyokubaliana katika mkutano uliofanyika Maputo mwaka 2003 uliopendekeza pia kuwa nchi za Afrika ziwe zimefanikiwa kukabiliana na Baa la Njaa na Utapiamlo ifikapo mwaka 2025.
Katika maelezo yake, Mheshimiwa Makamu wa Rais alifafanua kuwa Tanzania imepiga hatua katika kilimo kupitia mpango wa Kilimo Kwanza na pia mpango wa kukuza uzalishaji kwa kutumia kanda maalum maarufu kama SAGGOT (unaojumuisha mikoa iliyo na uwezo wa kuzalisha chakula kwa wingi) umeanza kukubalika na kuwa mpango wa nchi nyingi za Afrika. Hata hivyo Mheshimiwa Makamu wa Rais alifafanua pia kuwa, ukuzaji wa Kilimo unapaswa kuambatana na sekta nyingine kama Nishati, Miundombinu, Viwanda na Biashara.
Umuhimu wa kukuza sekta hizo unatokana na ukweli kuwa, zinachangia kukuza kilimo, kukifanya kuwa na tija na pia kutoa unafuu wa uzalishaji kwa wakulima. Tena kwa kukuza sekta hizo, Afrika inaweza kupiga hatua kubwa kwani tatizo la uzalishaji halitokani na upungufu wa uzalishaji tu, bali hata pale panapokuwa na uzalishaji mkubwa, kuna maeneo ambayo mazao yameshindwa kulifikia soko ama kufikishwa kwa watu wenye mahitaji.
Awali akichagia katika mkutano huo, Rais Mstaafu wa Brazil Lula da Silva alisema njaa ni jambo la kijamii, linalochangiwa kwa kiasi kikubwa na binadamu wenyewe hasa pale mtaji na kipato kinapobakia kuwa katika mikono ya wachache wakati wengi wakiambulia patupu.
Rais Lula pia alimnukuu Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kusema; “kama mnataka maendeleo lazima mshirikishe wananchi wote.” Kwa kutumia nukuu hii, Rais Lula anasisitiza kuwa, Afrika inapaswa kuwa na mipango inayoshirikisha wananchi ili iwasaidie kukua kiuchumi na kukabiliana na matatizo yanayowakabili katika maisha yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika Dk. Nkosazana Zuma alisema barani Afrika kuna changamoto kubwa inayowakabili akina mama na moja ni kubwa ni kukosa fursa ya kumiliki ardhi hali inayofanya uzalishaji kuwa duni. “Jambo hili linaweza kubadilishwa na sisi, tunaweza kubadili tamaduni zetu kwa kuwa tunatambua mchango mkubwa wa akina mama katika Kilimo. Hata hivyo, kama hatutafanya mabadiliko akina mama watabakia nyuma na bara la Afrika litazidi kukabiliana na Baa la Njaa,” alisema.
Naye Rais Mstaafu wa Nigeria Olesegun Obasanjo aliueleza mkutano huo kuwa, zipo tamaduni barani Afrika ambazo zinawabagua wanawake japokuwa ndio wazalishaji zaidi. Pia akaongeza kuwa, wanawake wasitumike katika shughuli za kisiasa tu bali wawezeshwe ili kufanikisha azma ya Afrika kukabiliana na njaa.
Makamu wa Rais katika mkutano huo ameambatana na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Injinia Christopher Chiza pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mahadhi Juma Maalim. Katika Mkutano huo pia viongozi mbalimbali wamehudhuria akiwemo Rais Mstaafu wa Brazil Lula da Silva, Rais Mstaafu wa Nigeria Olesegun Obasanjo, Rais Mstaafu wa Ghana John Kuofor.
Viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo ni Mkurugenzi wa Shirika la Chakula Duniani, Jose Graziano da Silva, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika Dk. Nkosazana Zuma, Rais wa Sudan, Benin na wawakilishi wa nchi mbalimbali ambazo ni wajumbe wa Umoja wa Afrika.