Mbunge aufagilia utendaji wa Serikali


Mbunge Neema Mgaya

Na Mwandishi Wetu

MBUNGE wa Viti Maalumu CCM, Neema Mgaya, ameipongeza serikali kwa kuwawezesha vijana wanaosoma elimu ya juu kupata mikopo na kuendelea na masomo yao.

Akichangia hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu, mwishoni mwa juma, Neema, alisema serikali imetumia sh. bilioni 185 kwa ajili ya kuwakopesha vijana 96,328, hapa nchini.

Sambamba na hilo, mbunge huyo anayewawakilisha vijana wa mkoa wa Dar es Salaam, alisema anaridhishwa na juhudi za serikali za kuwawezesha wananchi katika kuongeza ajira kupitia sera, mikakati na mipango mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kubuniwa.

“Naipongeza serikali yetu inayoongozwa na Rais Kikwete, kwa kubuni sera na mipango hiyo, kwani inalenga kuwawezesha wananchi wengi kupata ajira, lakini sijaona sehemu ambayo kijana ametajwa katika mipango hiyo,” alisema.

Alisema licha ya mipango na mikakati mizuri ya serikali kufungua milango kwa wananchi kupata ajira, changamoto kubwa iko kwa vijana ambao wanakabiliwa na tatizo kubwa la ajira.

Alisema upo umuhimu wa vijana wa Tanzania kuunda baraza lao la vijana litakalotoa nafasi kwa vijana kubadilishana mawazo na wenzao walio kwenye baraza la vijana la jumuia ya Afrika Mashariki, ili kuzungumzia changamoto zinazowakabili na kuona jinsi ya kukabiliana nazo.