IMEELEZWA kwamba kadri wanawake na wasichanana wanavyopata elimu zaidi ndivyo vifo vya kina mama wajawazito na watoto vinavyopongua, kuimarika kwa uzazi wa mpango na kipato cha familia kuongezeka.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea kwenye kikao cha wake wa Marais na Viongozi wa Serikali waliohudhuria mkutano wa Majadiliano kwa Manufaa ya Wote (Smart Partnership Dialogue) katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Katika kikao hicho mambo mbalimbali yalijadiliwa ikiwa ni pamoja na jinsi gani technologia inavyoweza kujipanga kusukuma mambo ya maendeleo katika jamii.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa kupatikana kwa elimu bora kutaisaidia jamii kuwa na afya bora, kukua kiuchumi, upatikanaji na ubora wa miuondombinu na nchi kuwa na maendeleo.
“Ni haki kusema kuwa watoto wa kike wakikosa nafasi ya kupata elimu wanakosa nafasi ya kuwa na maendeleo kwani asilimia 40 ya watoto ambao mama zao wamepata elimu ya msingi wameweza kuepukika na vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na asilimia 50 wameweza kupata chanjo mbalimbali.
Alisema kuwa ili kuhakikisha kwamba wasichana wanapata elimu Serikali ya Tanzania imeongeza idadi ya Shule ambazo zitaweza kuchukua watoto wengi zaidi. Kwa mwaka 2012 idadi ya watoto waliokuwa wanasoma shule ya msingi ilikuwa ni 8,247.172 sawa na asilimia 98.4.