MKURUGENZI Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Usu Mallya amefungua mafunzo ya Ukatili wa Kijinsia na Haki za Binadamu kwa kundi la washiriki kutoka mikoa na taasisi anuai za umma na binafsi ili kuwajengea uwezo juu ya mapambano ya masuala upiganiaji haki kwa jamii.
Akizungumza na washiriki wa semina hiyo, Bi. Mallya aliwataka washiriki kutumia nafasi waliopata ipasavyo kwa kuhakikisha wanafuatilia mafunzo vizuri ili kila mmoja atoke kama malozi wa chachu ya mapambano juu ya vitendo vyote vya kikatili kwa jamii na masuala ya haki za binadamu.
Aliwaeleza washiriki kila mmoja kwa nafasi aliyonayo sasa anaweza kuwa chachu ya mabadiliko endapo atatimiza wajibu wake kwenye eneo alipo. Alisema suala la ukatili wa kijinsia ni suala mtambuka nchini kwani limeenea karibuni kila eneo la nchi, hivyo kuna kila sababu ya kuzidisha mapambano dhidi yake.
“…Kwa kweli suala la ukatili wa kijinsia ni suala mtambuka kwenye maeneo yote ya nchi yetu, twakwimu za kitaifa zinatuambia takribani asilimia 40 ya wanawake wote wamekwisha fanyiwa ukatili wa namna moja ama nyingine, kwa kila wanawake wawili mmoja ameshafanyiwa ukatili wa kijinsia…wengine tumepigwa, wengine tumefanyiwa ukatili wa kiuchumi, kisaikolojia…,” alisema Mallya.
Aidha Mallya aliongeza kuwa ukatili wa kijinsia kwa sasa katika mfumo wa utandawazi lipo kila upande bila kujali ni kwa wanawake au wanaume, kwani kila mmoja anaathirika na suala hilo. Alisema lengo la mafunzo kama hayo ni kuona mabadiliko katika mfumo juu ya kujali na kuheshimu haki za makundi yote, yaani haki za watoto, haki za kijamii, haki za watu wenye ulemavu, haki za wanawake haki za vijana n.k.
Alisema kuwa nchi nyingi za Bara la Afrika zinapambana na mifumo miwili mikubwa, ambayo ni mfumo wa kitabaka unaoongeza nafasi kati ya matajiri na masikini (walio nacho na wasionacho) na mfumo dume ambao nao umekuwa ukiwakandamiza wanawake katika jamii.
Mafunzo hayo yanaendeshwa na Chuo cha Mafunzo ya Jinsia (GTI) ambacho kilianzishwa na TGNP ili kuratibu mafunzo anuai ya jinsia chini ya mwamvuli wa TGNP. Miongoni mwa washiriki katika semina hiyo ni wawakilishi kutoka madawati ya jinsia ya Jeshi la Polisi, mahakama, idara ya ustawi wa jamii, washiriki kutoka asasi za watu wenye ulemavu na wasio na ulemavu na baadhi ya wajumbe kutoka mikoa kadhaa ya Tanzania.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com