TIMU ya Makumbusho United imeanza vema mashindano ya vijana chini ya
umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars mkoa wa kisoka wa Kinondoni
baada ya kuibamiza timu ya Sifa United ya Manzese 3-1 katika mechi
iliyokuwa na ushindani mkubwa iliyopigwa kwenye uwanja wa Mwananyamala
shule ya msingi jijini Dar es Salaam leo Jumapili, Juni 23 2013.
Ilikuwa ni Sifa United walioanza kufunga goli katika dakika ya 16
wakati mchezaji wao hatari Jumbe Evon alipowatoka walinzi wa
Makumbusho United na kuachia shuti kali iliyotinga wavuni moja kwa
moja na kuibua hamasa kubwa kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo
waliofika uwanjani kushuhudia mchezo huo. Goli hili lilidumu hadi
mapumuziko.
Baada ya kupata maelekezo kutoka kwa kocha wao, wachezaji wa timu ya
Makumbusho United walikianza kipindi cha pili kwa kasi kubwa na juhudi
zao zilizaa matunda dakika tatu ndani ya kipindi cha pili wakati
mchezaji mwenye kasi Willy Kalolo alipoipatia timu yake goli la
kusawazisha.
Goli hilo la kusawazisha lilibadilisha kabisa sura ya mchezo huku
vijana wa Manzese wakipambana kupata goli la kuongoza lakini walinzi
wa Makumbusho walikuwa imara. Ilikuwa dakika ya 55 ambapo Makumbusho
waliandika goli la pili kupitia kwa Ally Amin ambaye alipiga shuti
kali na kuingia wavuni kabla ya Kalolo kufunga goli la tatu daikia ya
70 na kuzima ndoto za Sifa United za kushinda mechi hiyo
Michuano hiyo ya kusaka vipaji vya wanasoka chipukizi inaendelea kesho
Jumatatu Juni 24 katika uwanja huo huo ambapo timu ya Mtakuja Beach
itapambana na Sifa United.
Katika mkoa wa kisoka wa Ilala, Buguruni Youth Center (BYC) kesho Juni
24 watakuwa na kibarua kigumu watakapopambana na Bomubomu katika mechi
ya kukata utepe itakayofanyika kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa
Secondari jijini Dar es Salaam. Kila upande umetamba kwamba utaibuka
na ushindi.
Wakati michuano hii inaendelea, makocha watakuwa na kibarua kigumu cha
kuchagua wachezaji ishirini bora kuunda timu za mikoa kwa ajili ya
fainali za Taifa zitakazopigwa katika uwanja wa kumbukumbu ya Karume
jijini Dar es Salaam kuanzia julai 2 2013.
Mkoa wa Temeke ambao ndio mabingwa watetezi wa ARS Taifa wanatarajia
kuanza mashindano haya ngazi ya mkoa siku ya Jumanne Juine 25. Mikoa
mingine inayoshiriki Airtel Airtel Rising Stars mwaka huu ni Morogoro,
Mwanza, Mbeya, Tanga, Kigoma na Ruvuma.
Programu hii ya Airtel Rising Stars ni ya Afrika nzima likiwa na lengo
la kuendeleza na kukuza mpira wa miguu katika bara la Afrika kwa
vijana wanaochipukia waweze kupata nafasi ya kuendeleza vipaji vyao.
Fainali za ARS Taifa vile vile zitatumika kuchagua timu bora za
wavulana na wasichana ambao wataiwakilishaTanzania katika mashindano
ya kimataifa ambapo nchi mwenyeji wa michuano hiyo itatangazwa mwezi
ujao. Wachazeaji wengine watachaguliwa kwenda kwenye kliniki
itakayoendeshwa na makocha kutoka klabu maarufu duniani ya Manchester
United